Mkuu wa Majeshi Uganda ampa Bobi Wine saa 48 kujisalimisha Polisi

Dar es Salaam. Katika hatua iliyoibua taswira ya wasiwasi kisiasa nchini Uganda, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini humo (CDF), Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni mtoto wa Rais Yoweri Museveni, ametangaza kupitia mtandao wa X kumsaka kiongozi wa upinzani, Bobi Wine.

Katika taarifa hiyo iliyosambaa na kuzua mjadala mitandaoni leo Jumanne Januari 20, 2026, Muhoozi amempa Bobi Wine saa 48 kuhakikisha anajisalimisha kwa polisi.

Amesema iwapo Bobi Wine hatatimiza agizo hilo, atachukuliwa kuwa ni mhalifu, atatafutwa kwa operesheni za kihalifu.

Aidha, taarifa ya kumhusu Bobi Wine imekuja katika mfululizo wa taarifa nyingi ambazo Mkuu huyo wa Majeshi ya Uganda amekuwa akiziweka kwa nyakati tofauti tangu kumalizika kwa uchaguzi huo, akitaja operesheni za jeshi hilo kwa wahalifu na hatua linazochukua.

“Ninampa saa 48 kamili kujitokeza mbele ya Polisi, asipofanya hivyo tutamchukulia kama mhalifu au mkaidi na tutamkabili ipasavyo,” amesema Muhoozi kwenye ukurasa wake wa X.

Taarifa hiyo imeibua mjadala mkali mtandaoni na kimataifa, huku hali ya kisiasa nchini humo ikizidi kuingia katika sintofahamu kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Januari 15, 2026 ambao Rais Museveni alitangazwa mshindi kwa zaidi ya asilimia 70 ya kura.

Katika uchaguzi huo ambao Bobi Wine aliibuka mshindi wa pili kwa asilimia 24 ya kura zilizopigwa, kiongozi huyo wa Chama cha National Unity Platform (UNP), aliyakataa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi.

Katika hoja yake, Bobi Wine amesema matokeo hayo ni ya uwongo akidai kulikuwepo udanganyifu wa kura, kushindwa kwa mashine za kielektroniki na mashambulizi dhidi ya wapinzani katika maeneo mengi.

Kufuatia hatua hiyo, Ijumaa ya kuamkia siku ya matokeo kutangazwa, jeshi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama lilizingira na kuweka kambi nyumbani kwake, yeye akidai kutorokea mafichoni.

Hata hivyo, katika Taifa hilo la Afrika Mashariki, kumeendelea kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa Bobi Wine tangu zilipoenea taarifa kuwa amekamatwa kabla ya yeye mwenyewe kukanusha kupitia akaunti yake ya X kuwa alifanikiwa kutoroka kabla hajakamatwa.

Kufuatia hatua hiyo, amri ya Mkuu wa Majeshi, Muhoozi inaibua mjadala kama Bobi Wine atatii au la kwani awali alionyesha kutoridhishwa na utendaji wa jeshi hilo kuhusu usimamizi wa uchaguzi akisema “limefanya makosa ya jinai dhidi ya wananchi wa Uganda.”