NYOTA wa timu zinazoshiriki Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam (BDL), wanatarajia kuchuana katika mashindano ya kugombea Kombe la Ramadhani ‘Ramadhan Star League’.
Mashindano hayo yameandaliwa na Taasisi ya michezo ya Mchenga Academy kwa kushirikiana na Twiga Sport Promotion na yamepangwa kuanza Februari 20 mwaka huu kwenye Uwanja wa DonBosco Oysterbay, Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Michezo ya Mchenga Academy, Mohamed Yusuph aliliambia Mwanaspoti ligi hiyo inatarajiwa kushirikisha timu zisizopungua nane zikiwamo nne za wanawake.
Yusuph amesema timu hizo zitaundwa na kupewa majina ya timu na baadaye Kamati ya Mashindano na kiongozi wa timu watapanga nyota hao wacheze timu ipi.
Akizungumzia kuhusu majina ya timu, amesema watatangaza majina hayo hivi karibuni baada ya kamati ya Ramadhani Star League kukutana.
Aliongeza, mashindano hayo yatakuwa yakifanyika kwa wiki mara tatu, Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi na upande wa timu za wanaume zitagawanywa katika makundi mawili.
“Timu mbili za juu kwa wanaume na wanawake zitakazofanya vizuri kila kundi zitacheza nusu fainali. Tumepanga michezo itakayofanyika, ianze baada ya wachezaji wote kufuturu uwanjani hapo,” amesema Yusuph.
Baadhi ya mastaa wanaotarajia kushiriki michuano hiyo maalumu inayofanyika kipindi cha Mfungo wa Mwezi wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza mwezi ujao ni; Fotius Ngaiza, Brian Mramba, Mwalimu Heri, Amin Mkosa, Tyrone Edrward na Jonas Mushi.