Msigwa: Uwekezaji bandari waimarisha ufanisi, mapato

Dar es Salaam. Serikali imesema uwekezaji uliofanywa katika Bandari ya Dar es Salaam umeleta mafanikio makubwa kiuchumi, ikiwemo kuongezeka kwa mapato na kuboreshwa kwa ufanisi wa bandari.

Hatua hiyo imeifanya bandari kuendelea kuwa lango kuu la uchumi wa Tanzania na ukanda wa Afrika.

Hayo yamesemwa leo Jumanne Januari 20, 2026 na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, alipotembelea maeneo mbalimbali ya bandari hiyo kabla ya kuzungumza na waandishi wa habari.

Msigwa amesema uwekezaji huo umechangia kwa kiasi kikubwa ongezeko la makusanyo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), akieleza kabla ya mwaka 2020, wastani wa makusanyo ya kila mwezi ulikuwa ni Sh1 trilioni, lakini kwa sasa umefikia wastani wa Sh3 trilioni kwa mwezi.

Katika upande wa mapato ya bandari, Msigwa amesema maboresho yaliyofanyika yameongeza mapato ya bandari kutoka Sh6 trilioni kwa mwaka hadi kufikia Sh27 trilioni kwa mwaka, akibainisha kuwa hilo ni ongezeko kubwa linalothibitisha kuwa uwekezaji huo ulikuwa sahihi na wenye tija kwa Taifa.

Amesema mafanikio hayo ni utekelezaji wa moja kwa moja wa malengo ambayo Serikali ilijiwekea ilipoamua kuwekeza katika bandari, hususan kwa lengo la kuongeza mapato, kuboresha miundombinu na kuimarisha ushindani wa bandari za Tanzania katika ukanda wa Maziwa Makuu.

Msemaji huyo wa Serikali amekanusha madai kwamba Serikali iliuza bandari kama ambavyo imekuwa ikizushwa akisema kauli hizo ni za kupotosha umma na kupuuza ukweli wa kile kilichotekelezwa.

“Serikali haijauza bandari zake, bali imepangisha bandari zake kwa lengo la kuongeza mapato, kuboresha miundombinu na kuongeza ufanisi wa bandari zetu. Bandari bado ni mali ya Serikali na zitaendelea kubaki chini ya umiliki wa Serikali,” amesema.

Amesema hatua ya upangishaji imeiwezesha Serikali kunufaika na utaalamu, mitaji na teknolojia ya kisasa, huku ikibaki na jukumu la usimamizi na umiliki wa rasilimali hizo muhimu za Taifa.

Msigwa ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema bandari ni mhimili muhimu wa uchumi wa nchi, akisisitiza kuwa bila bandari zenye ufanisi, Taifa haliwezi kukuza uchumi wake kwa kasi inayohitajika wala kushindana kikanda na kimataifa.

Maboresho yaliyofanyika na ufanisi wake

Akizungumzia maboresho yaliyotekelezwa, Msigwa amesema Bandari ya Dar es Salaam imefanyiwa maboresho makubwa ya kuimarisha miundombinu, kuboresha mifumo ya uendeshaji na kuongeza uwezo wa kuhudumia meli na shehena.

“Bandari ya Dar es Salaam ni lango kuu la usafirishaji wa mizigo katika ukanda wa Afrika, ndiyo maana Serikali iliona ni lazima ifanye uwekezaji mkubwa ili kuondoa changamoto za muda mrefu na kuifanya bandari hii iwe ya kisasa na yenye ufanisi,” amesema.

Kwa mujibu wake, kabla ya maboresho hayo, bandari ilikuwa ikikabiliwa na changamoto za muda mrefu wa kuhudumia meli, msongamano wa meli nangani na uwezo mdogo wa kupokea meli kubwa.

Amesema hali hiyo ilikuwa inaongeza gharama za biashara na kupunguza ushindani wa bandari, akisisitiza kuwa baada ya uwekezaji, muda wa kuhudumia meli umepungua kwa kiasi kikubwa, idadi ya meli zinazohudumiwa imeongezeka na bandari sasa ina uwezo mkubwa zaidi wa kupokea na kuhudumia meli kubwa ikilinganishwa na hali ya awali.

Msigwa amesema maboresho hayo yameongeza pia ufanisi wa upakuaji na upakiaji wa mizigo, hali iliyosaidia kuongezeka kwa shehena zinazopita bandarini na kuimarisha nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafirishaji kwa nchi jirani.

Ameongeza ongezeko la ufanisi bandarini limeleta faida za moja kwa moja kwa Serikali kupitia mapato, lakini pia kwa sekta binafsi kupitia kupungua kwa gharama na muda wa biashara.

Lengo la uwekezaji na matarajio ya baadaye

Akieleza sababu za Serikali kuwekeza katika bandari, Msigwa amesema lengo lilikuwa ni kuifanya bandari iwe kichocheo kikuu cha uchumi wa Taifa, kuongeza mapato ya Serikali na kuweka mazingira bora ya biashara.

“Uwekezaji huu umeifanya bandari kuwa na uwezo wa kuhudumia meli kubwa zenye urefu wa mita 305 kutoka uwezo wa awali wa meli ya urefu wa mita 15 pekee,” amesema, akisisitiza hayo ni matokeo ya maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kuboresha miundombinu ya uchumi ili kuchochea maendeleo ya nchi.

Amesema pia Serikali inaendelea kuboresha bandari mbalimbali nchini sambamba na Bandari ya Dar es Salaam, zikiwemo Bandari ya Mwanza, Kigoma, Kemondo, Bukoba, Mbababay, Mtwara na Bandari ya Tanga, ambazo zote zimeongeza mapato na uwezo wa kuhudumia meli kubwa.

Akizungumzia maboresho yalivyoongeza uwezo wa kufanya kazi, Kaimu Mkurugenzi wa Bandari ya Dar es Salaam, Abeid Abeid amesema bandari hiyo imekuwa na ufanisi mkubwa katika kushusha mizigo kutokana na miundombinu ya kisasa na Tehama iliyowekezwa hapa.

“Awali, Bandari ya Dar es Salaam ilichukua siku 30 hadi 40 kuhudumia meli, lakini sasa ni wastani wa siku sita meli kubwa inahudumiwa kikamilifu,” amesema.

Akitoa msimamo wa Serikali kuhusu uwekezaji huo, Msigwa ameweka wazi kuwa mafanikio yaliyopatikana hadi sasa ni ushahidi kuwa uwekezaji uliofanywa ulikuwa sahihi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia na kuboresha bandari zote nchini ili kuhakikisha zinabaki kuwa nguzo imara ya uchumi wa Taifa na chanzo endelevu cha mapato ya Serikali na ajira.