WAKATI kikosi cha Yanga kikiondoka leo Jumatano jijini Dar es Salaam kuifuata Al Ahly, Misri kwa ajili ya mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Pedro Goncalves amesema hana presha yoyote kuhusu pambano hilo na kilichompa faraja kubwa ni ubora ulioongezwa na wachezaji wapya waliosajiliwa dirisha dogo msimu huu.
Pedro amesema ataingia kwenye mechi hiyo akiwa na imani kubwa baada ya kuona namna mastaa wapya walivyoanza na kuonyesha tofautikatika kikosi, hali iliyoongeza ushindani na wigo mpana wa machaguo.
Mashabiki wa Yanga jana Jumatatu walipata fursa ya kuwaona kwa mara ya kwanza wachezaji wapya, Mohamed Damaro, Allan Okello na Laurindo Aurelio ‘Depu’ wakicheza mechi ya Ligi Kuu Bara na waliisaidia kupatikana ushindi mnono wa mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa.
Pedro amesema ni jambo la kutia moyo kuona mchezaji anayejiunga katika dirisha dogo la usajili akiingia na kujaribu kuleta utofauti ndani ya timu.
“Hili ndilo tunalotaka, mchezaji aingie na aongeze kitu tofauti kwenye kikosi,” amesema Pedro aliyeiongoza Yanga katika mechi 10 za mashindano tofauti akishinda tisa na sare moja.
Kocha huyo alimtaja Damaro ameonyesha uwezo mkubwa wa kuimarisha uwiano wa timu katika eneo la kiungo, hasa kutokana na uwezo wake wa kucheza mbele ya mabeki wawili wa kati.
Kwa upande wa Okello, alionyesha ubora wake wa kiungo mshambuliaji baada ya kutengeneza nafasi tatu za wazi kipindi cha kwanza, kabla ya kupiga faulo iliyozaa bao la sita kwa Yanga dhidi ya Mashujaa.
Bao hilo lilifungwa na Depu, ambaye aliwavutia mashabiki wa Yanga kwa kasi, nguvu na ubunifu wake, ikiwa ni pamoja na asisti aliyotoa na harakati zake ndani ya boksi la Mashujaa.
Pedro amesema ushindani huo mpya ndani ya kikosi unawapa benchi la ufundi chaguo pana zaidi, hasa kuelekea michezo migumu ya kimataifa.
“Wachezaji wapya wanatupa suluhisho tofauti kulingana na aina ya mchezo,” amesema kocha huyo raia wa Ureno.
Yanga inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara kwa pointi 19 kabla ya JKT Tanzania haijacheza jana, pia inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Kundi B la Ligi ya Mabingwa Afrika ikikusanya pointi nne sawa na Al Ahly inayoongoza kwa tofauti ya mabao.
Katika mechi mbili walizocheza hatua ya makundi, Yanga haijaruhusu bao lolote, rekodi inayoongeza imani kabla ya safari ya Cairo kuifuata Al Ahly.