MWANAMITANDAO na shabiki maarufu wa klabu ya Manchester City, Brydon Bent, anatarajiwa kuwasili Tanzania katika kampeni za utalii #UnforgetableTanzania na #DestinationTanzania, hatua inayotarajiwa kuendeleza kuitangaza Tanzania kimataifa kupitia majukwaa ya kidijitali.
Brydon alijipatia umaarufu mkubwa hapa nchini miaka kadhaa iliyopita kutokana na video zake akiongea Kiswahili fasaha na kuonesha mapenzi makubwa kwa vivutio vya utalii vya Tanzania, jambo lililomfanya kupendwa na mashabiki wengi wa Kitanzania, hususan mitandaoni.
Licha ya kuwa amepitia kwenye academy za soka, Brydon kwa sasa ni mtangazaji wa vipindi vya watoto katika vyombo vikubwa vya habari nchini Uingereza, vikiwemo BBC Kids, Sky Kids, pamoja na Formula 1 Kids.
Aidha, ni mtangazaji wa mechi za Manchester City kupitia Man City TV, akihusishwa moja kwa moja na klabu hiyo anayoishabikia kwa dhati.
Mwaka 2024, Brydon aliweka historia kwa kushinda Tuzo ya British Academy Film Award (BAFTA), katika kipengele cha Mtangazaji Chipukizi, tuzo inayothibitisha ubora na ushawishi wake katika tasnia ya utangazaji.
Katika safari yake ya taaluma, Brydon amepata fursa ya kufanya mahojiano na mastaa wakubwa wa soka duniani, akiwemo Kocha Pep Guardiola, Sergio Agüero, Neyma na wengineo, hatua iliyompa heshima na kutambulika zaidi kimataifa.
Ujio wa Brydon Bent nchini Tanzania unatarajiwa kuwa chachu muhimu katika kutangaza utalii wa Tanzania kwa hadhira ya kimataifa, hususan kwa vijana na mashabiki wa soka, kupitia majukwaa ya kidijitali na mitandao ya kijamii.