Arusha. Mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei, na aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amefariki dunia.
Mzee Mtei (94) ambaye alikuwa Gavana wa BoT kuanzia 1966 na miaka 12 baadaye akaja kuwa Waziri wa Fedha na Mipango amefariki usiku wa kuamkia leo Januari 20, 2026.
Ameitumikia nafasi ya Waziri wa Fedha na Mipango kuanzia 1978 mpka 1981 alipojiuzulu wadhifa huo.
Akizungumza na Mwananchi asubuhi hii, Freeman Mbowe ambaye amewahi kuwa Mwenyekiti wa Chadema amesema, Mzee Mtei ameugua kwa kipindi kirefu na hali yake ilibadilika ghafla na wakati wanamchukua kwa gari la wagonjwa kumpeleka hospitali ya Seliani na kufariki dunia akiwa njiani.
Mbowe amesema hadi anafikishwa hospitali tayari Mzee Mtei alikuwa tayari amefariki dunia.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, John Heche, imeeleza kuwa chama hicho kimepoteza moja ya nguzo imara sana.
“Chama chetu kitatoa taarifa rasmi ya asubuhi (leo).Tunachukua nafasi hii kutoa pole sana kwa familia ya mzee Mtei, ndugu jamaa na marafiki,” amesema Heche katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii
“Chadema tumepoteza moja ya nguzo imara sana za chama chetu. Tutamuenzi Mzee Mtei kwa mema yote aliyoyafanya kwa chama na nchi yetu,” amesema Heche.
Pia, alikiasisi Chama cha Chadema mwaka 1992 na kuwa mwenyekiti wake wa kwanza ambapo amefariki dunia kikiwa kinaadhimisha miaka 33 tangu kipewe usajili.
Mzee Mtei alizaliwa Julai 12, 1932 Marangu, Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo kwa sasa msiba uko nyumbani kwake Tengeru, Arusha inapoendelea kufanyika mipango ya mazishi.
Endelea kufuatilia Mwananchi