Arusha. Mwili wa mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei anatarajiwa kuzikwa Jumamosi ya Januari 24, 2026 nyumbani kwake Tengeru nje kidogo ya Jiji la Arusha.
Mzee Mtei ambaye pia alikuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), alifariki dunia usiku wa Jumatatu, Januari 19, 2026 jijini Arusha, akiwa na umri wa miaka 94.
Melyi Mtei (57) ambaye ni mtoto wa nne kati ya watano wa Mzee Mtei, akizungumza leo Jumanne Januari 20, 2026 nyumbani kwao, amesema mazishi yatafanyika Jumamosi katika makaburi ya familia, Tengeru wilayani Arumeru.
“Baba amefariki jana usiku, alikuwa mzee na tunatarajia kumzika Jumamosi hapahapa shambani Tengeru,” amesema.
Melyi amesema baba yao alikuwa mtu mcheshi na ambaye alithamini sana elimu.
“Tutamkumbuka mzee wetu, alikuwa na upendo sana, alikuwa anatupenda sana familia kama watoto wake, alikuwa anapenda watu wasome, alithamini sana elimu,” amesema na kuongeza.
“Baba alikuwa mcheshi sana, alipenda kukaa na kila mtu na baada ya kustaafu alikuwa anapenda kuangalia kahawa shambani kwake, lakini umri ulivyokuwa unazidi aliacha akawa anakaa nyumbani,”amesema.
Amesema baadhi ya viongozi wenzake waliokuwa wakifanya naye kazi walikuwa wanafika nyumbani kumjulia hali ila muda unavyozidi kwenda nao waliendelea kupungua hawapo tena.
Akizungumza msibani hapo, Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Tottinani Ndonde amesema chama hicho kimepokea msiba huo kwa uzito mkubwa hasa ikizingatiwa msiba huo umetokea katika kipindi ambacho kilitarajia kuadhimisha miaka 33 tangu kipewe usajili.
Amesema katika kuenzi mchango wa Mzee Mtei, wamepanga Januari 22 na 23,2026 watafanya maadhimisho kuenzi mchango wa Mtei.
“Nitoe pole kwa wana Chadema na kwa msiba huu mzito na wapenda demokrasia wote kwa sababu marehemu Mtei amekuwa mwasisi wa wapigania demokrasia na leo nadhani Watanzania wanaona matunda yake amekuwa na mchango mkubwa sana.
“Ni jambo ambalo limetokea katika kipindi ambacho hatukukitegemea lakini tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Mzee Mtei. Katika kuenzi mchango wake kabla ya maziko tutakuwa na siku mbili na shughuli rasmi za kichama kumuenzi Mzee Mtei,” amesema.
Mzee Mtei ambaye alikuwa Gavana wa BoT kuanzia 1966 na miaka 12 baadaye akaja kuwa Waziri wa Fedha na Mipango kuanzia 1978 mpaka 1981 alipojiuzulu wadhifa huo.
Mzee Mtei, alizaliwa Julai 12, 1932 Marangu, Moshi mkoani Kilimanjaro ambapo msiba uko nyumbani kwake Tengeru, Arusha inapoendelea kufanyika mipango ya mazishi.