Dar es Salaam. Hoja ya ombwe la utawala wa sheria imeibua mjadala, baadhi ya wadau wamesema hali hiyo imesababishwa na baadhi ya mihimili kutotimiza wajibu kama inavyopaswa.
Wapo wanaosema hakuna ombwe la utawala wa sheria nchini, kwa hoja kuwa kila muhimili unatimiza wajibu wake wa kutunga sheria, kusimamia na kutekeleza, kadhalika kutafsiri.
Wanaosema kuna ombwe la utawala wa sheria wanatumia mifano ya matukio ya utekaji na kukosekana kwa uwajibikaji kuwa ishara tosha ya kuwepo watu walio juu ya sheria.
Chimbuko la mjadala huo ni kauli ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku, ya Januari 19, 2026, alipozungumza na waandishi wa habari, akisema Serikali inaonekana kushindwa katika utawala wa sheria.
“Vijana wetu wamelazimika kwenda mtaani. Nchi imeanza kushindwa, kwa hiyo leo hali ikoje. Tunakutana hapa kuzungumza hali halisi ya Taifa letu, tumefikaje katika msiba huu,” alisema.
Kwa sababu hiyo, alisema ameitisha kikao cha wazee kutafuta ukweli, kwa kuwa wanaona Taifa limeanza kushindwa kuishi katika mfumo wa sheria, na wanalenga kuliponya.
Wakati kukiwa na mitazamo hiyo, tume iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuangalia mfumo wa haki jinai iliwahi kupendekeza mambo kadhaa ili kuimarisha utawala wa sheria, ikiwemo mamlaka ya uteuzi wa viongozi ielekeze viongozi wote wasio na mamlaka mahsusi ya kisheria ya ukamataji kuzingatia taratibu zilizowekwa na sheria katika kutoa amri za ukamataji.
Pia, ilipendekeza baada ya maelekezo hayo kutolewa, na kiongozi yeyote kukiuka maelekezo hayo, kiongozi huyo awajibike yeye mwenyewe na Serikali isiwe sehemu ya shauri litakalotokana na ukiukwaji huo.
Kwa tafsiri ya mchambuzi wa siasa, Profesa Hamisi Luhanga, utawala wa sheria si kuwepo kwa sheria nyingi vitabuni, bali ni utii wa sheria hizo kwa kila mtu bila kujali mamlaka yake.
“Hii inaweka wazi tofauti iliyopo kati ya kuwepo kwa mfumo wa kisheria na utekelezaji wake kwa haki na usawa kwa kila raia, bila kujali ana cheo au hadhi gani,” ameeleza.
Kwa Tanzania, amesema kuna sheria za kutosha, mahakama na vyombo vya ulinzi na usalama, zote ni nyenzo za utekelezaji wa utawala wa sheria, lakini kuna tatizo.
Kwa mujibu wa mchambuzi huyo, tatizo lililopo ni baadhi ya mihimili kutotimiza wajibu wao kama inavyopaswa, hivyo kusababisha matukio ya uvunjwaji wa sheria.
“Kuna matukio ya utekaji, kupotea kwa watu, ubadhilifu, na hatua hazionekani zikichukuliwa. Hii ni kwa sababu kuna muhimili hautimizi wajibu wake, hilo pekee ni ombwe la utawala wa sheria,” amesema.
Mtazamo huo unatofautiana na ule wa Mwanazuoni wa Sheria wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Leonard Shaid, aliyesema haoni shida kwenye utawala wa sheria nchini.
“Ukisema kuna ombwe la utawala wa sheria, inapaswa useme muhimili gani hautimizi wajibu wake. Muhimili wa kutunga sheria unatunga, wa kutafsiri unatafsiri, wa kusimamia na kutekeleza unafanya hivyo, hakuna shida,” amesema Profesa Shaid.
Ameitaja Marekani, akisema inasifika kwa utawala wa sheria, lakini matendo yake ya karibuni (hakuyataja) yamewashangaza wengi.
Mtafiti wa masuala ya demokrasia, Dk Rehema Kalinga, amesema changamoto si kukosekana kwa sheria, bali ni kuchagua lini na kwa nani sheria itumike.
“Hapa ndipo ombwe linapoanza, kwenye utekelezaji wa sheria kwa upendeleo, jambo linalosababisha kuporomoka kwa imani ya wananchi kwa taasisi za dola,” amesema.
Katika mazingira hayo, amesema wananchi wanajikuta wakishuhudia baadhi ya watu wanakuwa juu ya sheria, huku wengine wakididimizwa zaidi.
Dk Rehema anaona chanzo cha tatizo hilo ni kulegea kwa mipaka kati ya mihimili ya dola, yaani Serikali, Bunge na Mahakama.
“Dhana ya usawa wa mihimili imekuwa ikitajwa mara nyingi kama nguzo muhimu ya utawala wa sheria, lakini kwa vitendo, mhimili mmoja umeonekana kuwa na uzito kuliko mingine,” amesema.
Mchambuzi wa siasa, Mwalimu Pius Mandari, amesema pale ambapo uteuzi, uhamisho au mustakabali wa viongozi wa taasisi muhimu unategemea zaidi ridhaa ya kisiasa kuliko uadilifu na weledi, utawala wa sheria hubadilika kuwa nadharia.
“Sasa hiyo ndiyo hali halisi ya Tanzania. Viongozi walioteuliwa mustakabali wao upo mikononi mwa ridhaa ya kisiasa, aliyemteua atamwondoa pale atakapotaka. Hakuwezi kuwa na utawala wa sheria kwenye hali hiyo,” amesema.
Mtaalamu wa Sheria, Hellen Kijo Bisimba, amesema tatizo la utawala wa sheria limechochewa na watu kuvunja sheria na kuachwa bila kuchukuliwa hatua.
“Mfano, haya mambo ya kutekwa yalianza kidogo kidogo. Watu wanatekwa mmoja mmoja, mwisho ikafikia wengi wanatekwa na hakuna mtu anayefuatilia.
Ili kutokomeza hali hiyo,” amesema, “Watanzania wanapaswa kuwa wa kweli, na aliyekosa aombe msamaha.
“Hivi sasa tunazungumza kutafuta amani. Swali la kujiuliza ni kwa nini amani iliondoka? Jibu ni jepesi, tulikwenda kusipotakiwa. Tunahitaji kuongea ukweli na tuondoe sintofahamu na maumivu yaliyotokea,” amesema.
Amesema Tanzania si nchi ya kwanza kupitia hali inayoipitia, zilikuwepo nchi zilizopita katika nyakati kama hizo, lakini walimaliza kwa kutafuta suluhu ya kweli, waliokosea wakatubu, amani ikarudi.
Mhadhiri wa zamani wa UDSM, Profesa Azaveli Lwaitama, amesema nchi ilionekana kulegea katika utawala wa kisheria kutokana na matukio ya utekaji na kamatakamata.
“Msingi wa yote tujiulize kwanza kulitokea nini? Tukubali kuna kitu kimetokea, na si kuanza kuwaza tumerogwa au kuna mchawi. Hatutaweza kupona,” amesema.
Amesema baadhi ya watu walijaribu kushauri na kupendekeza nini kifanyike, wakapuuzwa, na sasa kila mmoja angalau anafahamu imekuwaje nchi ikafika ilipofika.
Amesema Taifa linapaswa kujinyenyekeza, Serikali iliyopo madarakani ikubali kusuluhishwa na wasuluhishi kutoka nje.
“Hapa tulipo tumekwama, tunakokwenda hakuendeki. Tukiendelea hivi basi kutakuwepo na ukimya tu, lakini hakuna amani,” amesema.