Polisi Watoa Ufafanuzi Kuhusu Video ya Askari Kupambana na Mtuhumiwa Benki

Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Tarime/Rorya limetoa ufafanuzi kuhusiana na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha Askari wa Jeshi la Polisi akipambana na mtu mmoja huku akiwa na bunduki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma Januari 19, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, tukio hilo lilitokea Januari 15, 2026 majira ya saa nane mchana katika Benki ya CRDB Tawi la Sirari, wilayani Tarime.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa mtu anayetajwa kwa jina la John Kohe Amosi, mkazi wa Kijiji cha Sokoni, Sirari, alifika katika benki hiyo akiwa na nia ya kutoa fedha licha ya kutokuwa na akaunti.

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa huyo aliingia ndani ya benki hadi eneo la wahudumu (bank tellers) akiwa amebeba begi dogo na kuanza kuwatishia kwa nguvu wahudumu akitaka apewe fedha bila kufuata taratibu za kibenki.

Hali hiyo ilisababisha taharuki ndani ya benki, na askari waliokuwa zamu walilazimika kuingilia kati na kumtaka mtuhumiwa huyo atoke nje na kutii amri.

Hata hivyo, wakati askari alipokuwa akijaribu kumtoa nje, mtuhumiwa aliripotiwa kumvamia askari mmoja kwa lengo la kumpokonya silaha, hali iliyosababisha askari kutumia nguvu kumdhibiti na hatimaye kumtoa nje ya benki na kumtia mbaroni.

Jeshi la Polisi limeeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa mtuhumiwa hana akaunti katika Benki ya CRDB, na uchunguzi wa kina unaendelea ili kubaini nia yake halisi na kama alikuwa na mshirika au dhamira nyingine za kihalifu, kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa.

🔴 Tufuatilie kupitia YouTube ya Global TV, like, comment ili kuendelea kuhabarika kila siku kwa habari mbalimbali zenye ukweli na uhakika.