Rais Samia aomboleza kifo cha mwasisi wa Chadema

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi baada ya kifo cha mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edwin Mtei (94).

Mtei aliyekuwa Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Januari 20, 2026 jijini Arusha, akiwa na umri wa miaka 94.

Ingawa umaarufu wa jina lake, unabebwa zaidi na nasaba yake na Chadema, kutokana na kuwa miongoni mwa wanachama wa mwanzo, Mtei ana historia ndefu pia katika utumishi wa umma.

Mwanasiasa huyo mkongwe nchini, amewahi kuwa Gavana wa BoT na ndiye wa kwanza kushika wadhifa huo tangu kuanzishwa kwa benki hiyo.

Mwanazuoni huyo wa uchumi pia, amewahi kuwa Waziri wa Nchi, Mipango na Uchumi wa Serikali ya Tanzania mwaka 1978, wadhifa aliodumu nao hadi mwaka 1981.

Utumishi wake ulivuka mipaka ya Tanzania, amewahi pia kuwa Katibu Mkuu wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki (EAC).

Rais Samia ametuma salamu hizo, leo Jumanne Januari 20, 2026 kupitia taarifa iliyotiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Rais Samia amepokea kwa masikitiko, taarifa za kifo cha Mzee Edwin Mtei.

“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa niaba yangu binafsi, natuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, na wote walioguswa na msiba huu,” imeeleza taarifa hiyo ikimnukuu Rais Samia.

Amesema alimkumbuka Mtei kama mmoja wa watumishi na viongozi wenye mchango katika ujenzi wa Taifa kwenye eneo la fedha, mipango na uchumi.

Amesema Mtei amehudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania mwaka 1966 hadi 1974 na kushiriki kuimarisha misingi ya uendeshaji wa Benki Kuu na uthabiti wa mfumo wa fedha nchini.

Amesema Mtei ataenziwa katika historia ya siasa za vyama vingi kama miongoni mwa waasisi wa demokrasia ya ushindani wa vyama, akitajwa kuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa Chadema.

Rais Samia amesema mchango wa Mtei utaendelea kukumbukwa na kuenziwa na vizazi vya sasa na vijavyo, hususan kupitia maandiko yake binafsi yanayoeleza safari yake ya maisha na utumishi wake katika kuijenga Tanzania.

Katika salamu zake hizo, Samia amewaombea faraja, nguvu na amani familia, ndugu na wafiwa wote na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi.