Arusha. Serikali imewataka wafanyabiashara nchini kuimarisha ushirikiano na taasisi za umma kwa kutumia majukwaa ya mazungumzo kama njia kuu ya kutatua changamoto zinazowakabili ili kuepuka migogoro ya mara kwa mara.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, Januari 19, 2025 jijini Arusha kwenye kikao kati ya Serikali na uongozi wa wafanyabiashara kwa lengo la kusikiliza changamoto zao, na kujadili suluhu za pamoja kwa kushirikiana na mamlaka husika, na uongozi wa wilaya.
Kikao hicho ni mwendelezo wa majadiliano yanayolenga kupata suluhu ya kudumu kufuatia mvutano wa hivi karibuni uliosababisha wafanyabiashara zaidi ya 14,000 jijini Arusha kutishia kuitisha mgomo usio na kikomo, wakishinikiza Serikali kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga, wanaopanga bidhaa zao kwenye barabara zilizo mbele ya maduka.
Katika kikao hicho, Londo amesema kuwa meza ya mazungumzo ndiyo njia bora ya kuwasilisha kero, mapendekezo na maboresho ya mazingira ya ufanyaji biashara bila kuathiri mnyororo wa thamani wa shughuli za kiuchumi.
“Serikali inatambua mchango mkubwa wa wafanyabiashara katika uchumi wa Taifa letu, ndiyo maana tunaendelea kuboresha mazingira ya biashara ikiwemo ujenzi wa masoko, kuimarisha mifumo ya mawasiliano na utoaji wa huduma.”
“Niwaombe basi, pale panapojitokeza changamoto, ni vyema kuziwasilisha mapema ili zifanyiwe kazi, kuliko kuingiza nchi katika migongano,” amesema Londo.
Ameongeza kuwa Serikali inafahamu baadhi ya kero zinazowakabili wafanyabiashara na iko tayari kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu ikiwemo maboresho ya masoko na miundombinu yake, hivyo kuwataka wafanyabiashara hao kuwa na subira.
Pia amewataka wafanyabiashara hao kutimiza wajibu wao wa msingi ikiwemo kulipa kodi na kufuata sheria, kanuni na taratibu za biashara nchini ili kufanya uchumi shirikishi na jumuishi.
Pia ametumia nafasi hiyo kuwataka maofisa wa mapato na halmashauri kuzingatia utu na ubinadamu wanapotekeleza majukumu yao.
“Kabla ya kuchukua hatua za kisheria, jitihada za kusaidia na kusikiliza zionekane, namaanisha mtu apewe nafasi ya kujieleza, na hatua zinazochukuliwa zisimdhalilishe na kutweza utu wake, maana changamoto za kiuchumi hazina mwenyewe.”
Katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Arusha, Adolf Locken, amesema kero kubwa inayowakabili mbali na manyanyaso ya maofisa biashara na mapato pia machinga kupanga bidhaa mbele ya maduka na kuziba njia za kuingia.
Amesema hiyo, inasababisha kupungua kwa wateja na ushindani usio sawa wa kibiashara kwa mujibu wa leseni zao na utitiri wa mapato wanayolipa serikalini.
“Zaidi ya wafanyabiashara 14,000 tuliamua kugoma kushinikiza kuondolewa kwa machinga mbele ya maduka yetu maana wanaziba hadi milango na mbaya zaidi wanauza bidhaa zilezile tunazouza sisi, huku sisi tukilipa kodi, pango na ushuru mbalimbali,” amesema Locken.
Ameongeza kuwa licha ya kuwasilisha malalamiko yao mara kadhaa katika ofisi za uongozi wa jiji na wilaya, maelekezo na ahadi zimekuwa nyingi bila utekelezaji.
“Mgomo ulikuwa hauna kikomo hadi tupate muafaka wa vitendo, tumekuwa tukihisi kuonewa na kutosikilizwa,” amesema.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema amefanikiwa kutuliza mgomo huo ili kupisha majadiliano ya kina yatakayotoa suluhu ya kudumu na kuzuia mgogoro huo kujirudia.
Amesema ataitisha kikao maalumu kitakachowakutanisha wafanyabiashara na uongozi wa halmashauri, hususan vitengo vya biashara, mapato na sheria, ili kushughulikia hoja zote zilizowasilishwa.
Katika hatua za awali, Mkude amesema ameagiza machinga kuondolewa barabarani na kuelekezwa kufanya shughuli zao katika maeneo yaliyotengwa rasmi yakiwemo masoko ya Machame, Ulezi, Kilombelo, Samunge na Majengo ya Juu.