TANESCO RUVUMA YAHIMIZA WANANCHI KULINDA NA KUTUNZA MIUNDOMBINU YA UMEME

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) mkoani Ruvuma limewahimiza wananchi na watumiaji wa umeme kuhakikisha wanalinda na kutunza miundombinu ya umeme iliyopo katika maeneo yao ili huduma ya umeme iendelee kupatikana kwa uhakika kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Wito huo umetolewa na Afisa Uhusiano Huduma kwa Wateja wa TANESCO mkoani Ruvuma, Alan Njiro, wakati akitoa elimu kwa wananchi wa kijiji cha Selekano kilichopo katika kata ya Liganga, Halmashauri ya Wilaya ya Songea.

Akizungumza na wananchi hao ambao vitongoji vyao vimepitiwa na mradi wa REA, Njiro amewataka kushiriki kikamilifu katika utunzaji wa nguzo, nyaya na miundombinu mingine ya umeme ili kuepuka uharibifu unaoweza kusababisha kukatika kwa huduma ya umeme.

Aidha, amewasisitiza wananchi kuwa waangalifu katika malipo ya kuunganishiwa umeme, akieleza kuwa gharama ya kuunganishiwa umeme vijijini ni shilingi elfu ishirini na saba (27,000) tu, na kuwataka kuepuka kutoa fedha kwa watu kwani malipo yote hufanyika kupitia namba za kumbukumbu ya malipo.

Amesema TANESCO itaendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha huduma ya umeme inalindwa na inawanufaisha wananchi katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.