Ufunguzi wa majengo ya taaluma na utawala katika Taasisi ya Sayansi za Bahari (IMS), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Zanzibar ni uthibitisho kwamba sasa Tanzania imejipanga kuwekeza katika mafunzo na utafiti wa rasilimali za pwani na bahari.
Uzinduzi huo uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika taasisi hiyo, eneo la Buyu Unguja Zanzibar Januari 8, 2025, ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali kuwekeza katika elimu, sayansi na maendeleo ya rasimali watu hususani katika sekta ya bahari au uchumi wa buluu.
Ujenzi wa majengo hayo yaliyotumia Sh11 bilioni, ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET), ambazo ni jitihada za Serikali katika kuleta mageuzi ya uchumi hususani katika maeneo ya sayansi za bahari na uchumi wa buluu.
Taasisi ya Sayansi za Bahari ilianzishwa Oktoba 17, 1978 baada ya kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki, ikirithi mali na eneo la East African Marine Fisheries Research Organization (EAMFRO) pale Mizingani Zanzibar na kukabidhiwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo IMS ilipewa majukumu ya kufanya utafiti, kuendesha masomo ya uzamili na kutoa huduma za ushauri.
Akizungumza wakati wa kuzindua majengo hayo, Rais Samia alisema Taasisi ya Sayansi za Bahari ni taasisi ya kimkakati, kwa kuwa mustakabali wa maendeleo unahusiana moja kwa moja na bahari.
Alisema taasisi hiyo inaendelea kuwa nguzo muhimu kwa kazi za kitafiti za sayansi za bahari ikichangia katika uvuvi endelevu, hifadhi za mazingira ya bahari na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, utalii wa bahari pamoja na uchumi wa buluu kwa ujumla.
“Uwekezaji huu utasaidia kuchochea na kufikia uchumi jumuishi, tafiti na maarifa yatakayozalishwa chuoni hapa yatasaidia uamuzi wa sera unaolinda rasilimali za bahari, sambamba na kuongeza tija na kipato cha wananchi kwa kizazi cha sasa na kijazo,” anasema Rais Samia
Anasema maendeleo ya taasisi hiyo hayapaswi kubaki ndani ya mipaka ya chuo pekee, jamii inayozunguka lazima inufaike na chuo kupitia ajira, huduma biashara na shughuli za kijamii itakayochagia kipato chao.
Anasema taasisi inapaswa kuwa kichocheo cha maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi, hivyo waanzishe na kuimarisha mafunzo mafupi ya vitendo kwa wananchi wanaojishughulisha na rasimali za bahari.
Anasema ni matarajio ya Serikali kwamba taasisi itaendelea kuwa mdomo wa Serikali katika maendeleo ya uchumi wa buluu, mshauri wa kisayansi katika masuala ya bahari na mazingira ya pwani na kitovu cha utafiti za kimataifa.
Anasema wataendelea kuwekeza katika elimu ya juu kama Dira ya Maendeleo ya 2020/50 inavyoelekeza, hususani katika kujenga uchumi shindani na uchumi shirikishi.
Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Jakaya Kikwete, alisema uwapo wa taasisi hiyo, kunaifanya kuwa kituo pekee mahiri ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, kwani hakuna kituo kingine chenye umahiri kama hicho katika masuala ya utafiti wa rasilimali za bahari.
Alisema kituo hicho ni mdau muhimu kwa Serikali na taifa katika maendeleo ya sayansi za bahari, mazingira ya pwani na mambo mengine yanayohusu uchumi wa buluu kwa ujumla.
Kikwete anasema mafunzo yanayotolewa na tafiti zinazofanywa katika taasisi hizo, ni mambo yenye manufaa kwa Tanzania na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki na dunia nzima.
“Majengo hayo sio miundombinu tu bali ni msingi muhimu kuendeleza utafiti, kutoa mafunzo bora na kuchangia katika kukuza uchumi wa buluu pamoja na maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla,” anasema
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa William Anangisye anasema Taasisi ya Sayansi za Bahari ni kitovu cha elimu, utafiti na ubunifu chini ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, chenye dhamira ya kuendeleza uchumi wa buluu kupitia maandalizi ya rasilimali watu wenye ujuzi katika sekta za bahari na ukanda wa pwani.
Anasema taasisi hutekeleza jukumu hili kwa kutumia mitalaa inayokidhi mahitaji ya kitaifa na kimataifa, kufanya utafiti katika nyanja mbalimbali za bahari na kutoa programu za shahada za awali na shahada za uzamili.
Anasema mwaka wa masomo 2006/2007 ilianza kudahili wanafunzi wa shahada za uzamili lakini kadri mahitaji ya wataalamu yalivyoongezeka sambamba na utekelezaji wa Sera ya Uchumi wa Buluu, taasisi ilipendekeza kuanzishwa kwa shahada ya awali.
“Hata hivyo, eneo la Mizingani halikuwa na nafasi ya kupanua majengo, jambo lililosababisha chuo kutafuta eneo jipya. Ndipo safari ya IMS ikafika Buyu, ambapo kwa juhudi za Serikali ujenzi wa miundombinu muhimu, ikiwemo jengo la taaluma na utawala, umekamilika kwa awamu ya kwanza,” anasema
Kwa mujibu wa Profesa Anangisye, kuanzia mwaka wa masomo 2019/2020, kwa mara ya kwanza, IMS ilianza kudahili wanafunzi wa shahada ya awali, yaani Bachelor of Science in Marine Sciences (BSc Marine Sciences).
Uanzishaji wa shahada hii umeweka msingi wa kupanua programu zaidi katika ngazi mbalimbali ikiwemo Cheti na Diploma, ili kukidhi mahitaji ya jamii na kuimarisha mchango wa taasisi katika utekelezaji wa sera ya uchumi wa buluu kwa maendeleo ya Taifa.
Anasema, uwekezaji uliofanyika ni sehemu ya utekelezaji wa dhima ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ya kuzalisha maarifa yenye mchango wa moja kwa moja katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia ndani na nje ya Tanzania, ambapo dhima hiyo inatekelezwa kupitia mpango mkakati wa chuo unaolenga kuboresha mifumo ya ufundishaji, ujifunzaji, utafiti na ubunifu, sambamba na kuimarisha utafiti wa bahari na uchumi wa buluu kwa manufaa ya Taifa.
Anataja manufaa ya uwekezaji huo ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya wanafunzi ambapo kwa sasa IMS ina uwezo wa kudahili takribani wanafunzi 172 kwa mwaka, lakini kutokana na kukamilika kwa ujenzi huu, itaongeza uwezo mara dufu na kufikia wanafunzi 472 sawa na ongezeko la wanafunzi 300 kwa mwaka.
Faida nyingine kupitia uwekezaji huo, wanataaluma watapata fursa za ubadilishanaji maarifa na uzoefu.
“Kukamilika kwa mradi huu kutaimarisha nafasi za kuwaambatisha wanataaluma (industry attachments) katika kampuni na taasisi za kazi na biashara zinazohusiana na taaluma zao, ili kupata uzoefu wa vitendo. Pia Chuo kitakuwa na fursa ya kupokea wataalamu wabobezi kwa ajili ya kubadilishana maarifa na uzoefu na wanataaluma pamoja na wanafunzi,” anasema.
Kadhalika anasema wanatarajia kuimarika kwa utafiti ambapo chuo kitaongeza uwezo wake wa kuchangia maendeleo ya Taifa kupitia tafiti mbalimbali, hususan katika eneo la uchumi wa buluu, jambo litakalosaidia kuendeleza maarifa na kutoa suluhisho kwa changamoto za kitaifa, katika ngazi zote.
Anaeleza faida nyingine kupitia uwekezaji huo, ni kuongezeka kwa ubora wa ufundishaji na ujifunzaji, kupitia maabara za kisasa, hatua itakayosababisha kuzalisha wahitimu wenye ujuzi na umahiri wa hali ya juu, wanaokidhi mahitaji ya soko la ajira.
“Kwa hatua tuliyoifikia, IMS sasa inaingia awamu mpya ya maendeleo baada ya leo kuzindua rasmi miundombinu ya kisasa hapa Buyu, pamoja na kuimarisha vituo vya Mizingani na Pangani. Miundombinu hii, inayojumuisha maabara, kumbi za mihadhara na vifaa vya kisasa vya mafunzo na utafiti, itaongeza uwezo wa taasisi kufundisha na kufanya tafiti na bunifu,” anasema.
Kwa mujibu wa Profesa Anangisye, kukamilika kwake kunafungua fursa ya kuanzishwa kwa programu mpya sita za kitaaluma zinazolenga mahitaji ya sekta za bahari na ukanda wa pwani.
Baadhi ya wadau wa elimu na utafiti wamepongeza hatua ya kuboresha miundombinu ya taasisi hiyo, wakisema ni wakati mwafaka kwa Serikali kujikita katika sekta ya uchumi wa buluu.
Omar Said Haji ni mtaalamu wa masuala ya utafiti anayesema hakuna maendeleo wala suluhisho la matatizo, iwapo hakuna tafiti zinazofanyika, hivyo kutolewa kwa programu hizo kutazalisha wataalamu wengi watakaotoa mchango kwa Taifa.
“Kutolewa kwa programu hizi kutawezesha kuzalishwa kwa wataalamu watakaotoa mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi wa buluu na ustawi wa Taifa kwa ujumla,” anasema.
Anaeleza hiyo ni fursa muhimu kwa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla, kuongeza ujuzi na maarifa katika kusoma hususani katika kipindi hiki ambacho Serikali imejizatiti kuendeleza masula ya uchumi wa buluu ambayo yana fursa nyingi ndani yake kwani yanahusisha takribani sekta tano tofauti.
Sekta zinazohusiana na uchumi wa buluu ni pamoja na utalii, ulinzi wa bahari, usafiri na usafirishaji baharini, uvuvi na mafuta na gesi.