Msumbiji. Umoja wa Mataifa umesema taribani watu 500,000 wameathiriwa na mafuriko katika maeneo ya kusini na kati ya Msumbiji kutokana na mvua kubwa zilizonyesha kuanzia katikati ya Desemba na kusababisha maafa katika mikoa ya Gaza, Maputo na Sofala.
UN imezitaja nchi zingine zilizokubwa na mafuriko hivi karibuni ni Tanzania, Afrika Kusini, Zimbabwe, Malawi, Zambia, Botswana, Lesotho na Eswatini.
Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq ametoa taarifa hiyo jana Jumatatu Januari 19, 2026 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wakati akieleza kuhusu juhudi mbalimbali za misaada ya kibinadamu katika maeneo yaliyoathirika.
Amesema mafuriko hayo yamesababisha uharibifu wa vituo vya afya na barabara, huku takribani kilomita 5,000 za barabara zimeharibiwa katika mikoa tisa.
“Barabara kuu inayounganisha mji mkuu, Maputo na maeneo mengine ya nchi sasa haipitiki,” amesema Haq.
Haq amesema shughuli ya kuwaondoa wakazi katika maeneo yalitoathirika zaidi inaendelea, ambapo vimetengwa vituo 50 vya muda vya malazi vinawahifadhi zaidi ya watu 50,000 kote nchini.
“Fedha za ziada zinahitajika kwa dharura ili kuendeleza juhudi za kibinadamu,” amesisitiza Haq.
Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo ameahirisha safari aliyopanga kuhudhuria Jukwaa la Uchumi Duniani nchini Uswisi, kutokana na mafuriko hayo.
Mamlaka nchini humo zimetangaza kuwa takribani asilimia 40 ya Mkoa wa Gaza imefunikwa na maji baada ya mvua kunyesha mfululizo kwa wiki kadhaa.
Gavana wa Gaza, Margarida Mapandzene Chongo amesema takribani watu 327,000 wanahifadhiwa katika makazi ya muda kama shule na makanisa.