Wadau wahoji muundo wa SUK, wasisitiza masilahi ya Taifa

Dar es Salaam. Wadau wa siasa nchini wamevishauri vyama vya CCM na ACT-Wazalendo upande wa Zanzibar kuweka kando masilahi ya vyama vyao na badala yake kutanguliza masilahi mapana ya Taifa, ili kufanikisha uundwaji na uendelevu wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Wadau hao wamesema ili SUK iwe na taswira halisi ya umoja wa kitaifa, ni muhimu iwashirikishe wadau wote vikiwemo vyama vyote vya siasa pamoja na raia wasio wanachama wa vyama vya kisiasa.

Ushauri huo unakuja kufuatia msimamo wa ACT-Wazalendo wa kutotaka kuingia kwenye SUK, huku kikitangaza kuunda kamati maalumu ya kuchambua upya misingi, malengo na muktadha wa kuanzishwa kwa serikali hiyo.

Akizungumza na Mwananchi leo Januari 20, 2026  mchambuzi wa masuala ya siasa za Zanzibar, Ali Makame Issa amesema vyama hivyo havipaswi kuangalia masilahi ya vyama vyao pekee bali ya Taifa kwa ujumla, akibainisha kuwa mabadiliko yoyote yasiyozingatia masilahi ya wananchi yanaweza kuwa na athari kwa Wazanzibari wote.

“Si kwa sababu tu wameandika Katiba na wanafanya uchaguzi, bali waangalie masilahi mapana ya Taifa. Hali ikibadilika, hasara haitakuwa kwa CCM au ACT-Wazalendo pekee, bali kwa Wazanzibari wote,” amesema Issa.

Amesema kuwa mjadala wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa umejikita zaidi kwenye masilahi ya vyama viwili, bila kuwajumuisha wananchi wasio wanachama wa vyama na vyama vingine vya siasa.

“Hata serikali ya umoja wa kitaifa inapoundwa na vyama viwili pekee, haiwezi kutoa tafsiri pana ya umoja wa kitaifa, kwa kuwa wapo raia wasiokuwa wanachama wa vyama na pia kuna vyama vingine vya siasa,” amesema.

Kwa mujibu wa Issa, mfumo wa sasa wa SUK haujakidhi matakwa ya Wazanzibari wote kwa kuwa haujaweka utaratibu wa kuwashirikisha wananchi wasio wanachama wa vyama au walioko kwenye vyama vingine.

“Tatizo ni kuangalia umoja kwa jicho la uchaguzi pekee. Wanachama wa vyama hawazidi 500,000, wakati Zanzibar ina zaidi ya raia milioni 1.8,” amesema.

Ameongeza kuwa Tanzania ina vyama vya siasa 19 vilivyosajiliwa kikamilifu, lakini vinapofika kwenye maamuzi ya msingi havipewi nafasi stahiki.

“Inakuaje suala la umoja wa serikali linajadiliwa na CCM na ACT-Wazalendo pekee? Kama lengo ni kuleta umoja wa kitaifa, basi vyama vingine vihusishwe. Vinginevyo, isemwe wazi kuwa ni umoja wa vyama hivyo viwili,” amesema.

Issa ameonya kuwa mtazamo huo unaweza kuifanya SUK kukosa uhai, huku baadhi ya wadau wakitaka ivunjwe ili kupisha ushiriki mpana zaidi.

Kwa upande wake, mchambuzi wa siasa, Said Miraaj amesema mijadala ya SUK inapaswa kujikita zaidi kwenye nafasi za kisiasa kama Makamu wa Kwanza wa Rais na mawaziri, badala ya madai ya nafasi za kiutendaji kama makatibu wakuu na wakurugenzi.

“Hivi ni vyeo vya kiutendaji ambavyo vinahitaji utaalamu na vinaendeshwa kwa mfumo wa ajira. Nafasi za kisiasa kama ukuu wa mkoa au wilaya zinaweza kujadiliwa,” amesema Miraaj.

Amesema kupanua wigo wa ushiriki katika nafasi za kisiasa kutaleta taswira sahihi ya umoja, lakini fursa hizo zisielekezwe kwa ACT-Wazalendo pekee bali kwa vyama vingine pia.

Ameeleza kuwa ACT-Wazalendo itanufaika zaidi endapo itaingia katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa kuwa itakuwa karibu zaidi kushiriki katika maamuzi ya Serikali na kusimamia sera na sheria.

“Kwa sasa kuna maamuzi yanapitishwa bila wao kushirikishwa, kama suala la kura ya mapema, ambalo limekuwa likiwapa changamoto,” amesema.

Ameongeza kuwa kushiriki kwao kutawawezesha kuunda serikali kivuli yenye nguvu na kuwasilisha misimamo yao kwa niaba ya wanachama na wananchi wanaowaunga mkono.

Hata hivyo, amesema kutoshiriki kwao katika serikali kuna hasara kubwa ikiwemo kupitishwa kwa sheria na maamuzi wanayoyapinga.

“Ukibaki nje ya mfumo, unaonekana kama mpinzani sugu na mchochezi badala ya mshiriki wa ujenzi wa Taifa,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Ally Khatibu, amesema ni muhimu kwa ACT-Wazalendo kuwasilisha majina ya wawakilishi wake ili waruhusiwe kuapishwa na kuruhusu shughuli za kiserikali kuendelea.

Amesema kuunda kamati mpya ni kupoteza muda kwa kuwa masuala mengi yanayojadiliwa tayari yameainishwa kwenye Katiba, huku bado kukiwa na nafasi ya vyama kujadili hoja hizo kupitia majukwaa rasmi.

“Wananchi wanahitaji maendeleo, si migogoro ya kisiasa,” amesema Khatibu.

Ameongeza kuwa kushiriki kwa ACT-Wazalendo ndani ya Serikali kutawapa fursa kubwa zaidi ya kushinikiza mabadiliko wanayoyataka kupitia vyombo halali vya uwakilishi, badala ya kujitenga na mchakato wa maamuzi.