Kibaha. Zaidi ya wafanyabiashara ndogondogo 150 wa Mtaa wa Mailimoja A, Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani, wamepangiwa maeneo mapya ya kufanyia shughuli zao, hatua inayolenga kuwaondoa katika hatari waliyokuwa wakikabiliana nayo walipokuwa wakifanya biashara pembezoni mwa barabara ya zamani ya Morogoro.
Maeneo walikopangiwa wajasirimali hao ni jirani na stendi ya zamani ya Mailimoja Mjini Kibaha huku ikielezwa kuwa wataendelea kusalia hapo hadi manispaa hiyo itakavyoamua vinginevyo.
Ugawaji wa maeneo hayo umefanyika leo Jumanne, Januari 20, 2026, ambapo wafanyabiashara hao walionyesha furaha yao kubwa wakisema sasa wataendesha biashara katika mazingira salama zaidi, yenye nafasi na yanayowapa uhakika wa usalama wa maisha yao na wateja wao.
Baadhi ya wafanyabiashara walioshukuru uongozi wa Manispaa ya Kibaha kwa hatua hiyo ni pamoja na Mery Rose, Dako Shabani na Anna Mtei, ambao walisema uamuzi huo ni faraja kubwa na chachu ya kukuza kipato chao, kwani sasa wana uhakika wa kufanya biashara bila hofu.
Ugawaji wa maeneo hayo ulisimamiwa na Mwenyekiti wa Mtaa wa Mailimoja A, Athuman Mbaraka, akishirikiana na baadhi ya watendaji wa Manispaa ya Kibaha.
Akizungumza katika tukio hilo, Mbaraka amesema uamuzi wa kuwapangia wafanyabiashara maeneo mapya umetokana na tathmini ya hatari kubwa waliokuwa wanakumbana nayo katika maeneo ya awali.
“Mazingira yale hayakuwa salama kabisa. Tuliona ni muhimu kuchukua hatua mapema kulinda maisha ya wafanyabiashara wetu ambao ni mhimili muhimu wa uchumi wa familia na manispaa kwa ujumla,” amesema Mbaraka.
Wajasilimali hao wakiwa eneo walilohamishiwa wakigawiwa maeneo ya kufanyia biashara zao. Picha na Sanjito Msafiri
Amewahimiza wafanyabiashara hao kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa, ikiwemo kulipa ushuru wa Manispaa wa Sh500 kwa siku pamoja na kudumisha usafi katika maeneo yao ya kazi.
Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, wafanyabiashara hao wanatakiwa kuanza kufanya shughuli zao kuanzia saa kumi na mbili jioni hadi saa saba usiku, ili kuweka utaratibu na usalama katika eneo husika.