CRDB yaweka historia, yafungua tawi la kwanza Dubai

Dar es Salaam. Benki ya CRDB imeweka rekodi mpya katika sekta ya fedha nchini na ukanda wa Afrika Mashariki na Kati baada ya kuzindua huduma zake jijini Dubai, Falme za Kiarabu (UAE).

Hatua hiyo inaifanya kuwa benki ya kwanza kutoka Tanzania na ukanda huo kutoa huduma katika Kituo cha Fedha cha Kimataifa cha Dubai (DIFC), huku pia ikiashiria kufunguliwa kwa ukurasa mpya katika upanuzi wa kimataifa wa benki hiyo kubwa nchini.

Uzinduzi huo uliofanyika leo, Januari 21,2026 umewakutanisha viongozi wakuu kutoka taasisi za fedha za kimataifa, wawekezaji kutoka maeneo mbalimbali duniani pamoja na washirika wa maendeleo ya kifedha.

Hafla hiyo ya uzinduzi imeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza kwa niaba ya Rais, Waziri Kombo ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuendeleza dira ya uchumi ya Tanzania kupitia diplomasia ya uchumi, jitihada ambazo zimekuwa zikitekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita.

Balozi Kombo amesema kuingia kwa benki hiyo Dubai ni mkakati madhubuti, akitaja nafasi ya Dubai kama kitovu kikuu cha mitaji ya dunia pamoja na uwepo wa mfumo imara wa kifedha na udhibiti.

“Uwepo wa benki ya Tanzania nchini Dubai utaimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Falme za Kiarabu, ukichochea biashara ambayo tayari imefikia takribani Dola bilioni 2.5 za Marekani kwa mwaka,” amesema Waziri Kombo.

Kwa upande wake, Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk Juma Akili, amesema hatua hiyo inaashiria kukomaa kwa sekta ya fedha ya Tanzania.

“Hatua hii muhimu inaonesha ukomavu na kuongezeka kwa umahiri wa sekta ya fedha ya Tanzania, pamoja na uwezo wa taasisi zetu za ndani kushindana katika masoko ya fedha ya kimataifa,” amesema.

Kwa sasa, Benki ya CRDB inahudumia zaidi ya wateja milioni sita katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, ikiwa na jumla ya mali inayozidi Dola bilioni 9 za Marekani, na uwepo katika Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Kundi la Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema upanuzi wa benki kwenda Dubai ni hatua ya kimantiki katika mkakati wa kikanda unaotokana na jiografia ya uchumi wa Tanzania na ajenda ya muunganiko wa Afrika.

“Benki ya CRDB imejengwa katika misingi ya kufadhili ukuaji wa Tanzania. Jinsi ambavyo Tanzania imekuwa ikikua na kuwa lango la uchumi katika ukanda huu, ndivyo benki nayo imekuwa ikikua kikanda,” amesema.

Nsekela ameongeza kuwa, “Dubai sasa inatuwezesha kuunganisha mitaji ya kimataifa, Tanzania, na Afrika Mashariki na Kati.”

Katika uzinduzi huo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Neema Mori, amesema hatua hiyo inaakisi kuongezeka kwa imani kwa benki hiyo kufanya kazi kwa viwango vya juu zaidi duniani.

“Hiki ni kielelezo cha kauli kuhusu utawala bora, uwezo na uaminifu wa benki yetu kimataifa.

“Uwepo wa Benki ya CRDB Dubai unaonesha kuwa benki za Afrika zinaweza kuanzisha ushirikiano wa kimataifa huku zikiendelea kuzingatia vipaumbele vya maendeleo ya Afrika,” amesema.

Aidha, viongozi wa Mamlaka ya Huduma za Fedha ya Dubai (DFSA) wameikaribisha Benki ya CRDB katika Kituo cha Fedha cha Kimataifa cha Dubai (DIFC), wakibainisha kuwa uwepo wa benki ya liafrika yenye mizizi imara ya kikanda unaimarisha korido ya fedha kati ya Afrika na Mashariki ya Kati, na kuboresha mtiririko wa mitaji ya muda mrefu kuelekea masoko yanayochipukia.