KIUNGO wa zamani wa Simba na JKT Tanzania, Hassan Dilunga amekamilisha dili la kujiunga na TRA United akiungana na Mzamiru Yassin waliyecheza pamoja wakiwa Simba.
Dilunga ambaye ameitumikia JKT Tanzania kwa misimu miwili, mkataba na klabu hiyo umetamatika hivyo ametua TRA United akiwa mchezaji huru.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya TRA United kimethibitisha usajili wa kiungo huyo na kuweka wazi kuwa wanaamini ataongeza kitu ndani ya timu yao kutoka na uzoefu na ubora alionao.
“Ni kweli na ni muendelezo wa kuboresha kikosi chetu baada ya kubaini upungufu kwenye mechi chache tulizocheza na tunaamini maingizo mapya yatakuwa tija ya ubora wa TRA kwani yamezingatia mahitaji kutoka benchi la ufundi.
“Dilunga ni kiungo mshambuliaji na sisi dirisha hili tumepoteza mchezaji mmoja eneo hilo ambaye ametua Yanga, hivyo tunaamini ni chaguo sahihi ataweza kufanya mambo makubwa na tukasahau kama kulikuwa na mchezaji aliondoka hapo kabla,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema bado wanaendelea na maboresho, hivyo mashabiki wa timu hiyo wategemee sajili nyingine bora kwa lengo la kutengeneza timu yenye ushindani ambayo itatoa changamoto kwa wapinzani wao lakini pia itamaliza tano bora mwisho wa msimu.
Kiungo huyo mshambuliaji amewahi kupita kwenye klabu mbalimbali kama Mtibwa Sugar, Yanga, Simba, Ruvu Shooting, JKT Tanzania na sasa amejiunga na timu ya wakusanya mapato Tanzania, TRA United.