Oktoba 29, 2025, Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) iliendesha uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani katikati ya kutokuwepo kwa mawasiliano ya intaneti lakini kwa ufanisi iliyokuwa nayo, matokeo yalitangazwa ndani ya saa 72.
Ni kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano hayo kutokana na kuzimwa kwa intaneti kulikofanywa na Serikali, leo hii ninapoandika makala hii, ni vigumu kupata matokeo ya urais, wabunge na madiwani katika tovuti za hapa Tanzania.
Matokeo ya Rais ambapo Rais Samia Suluhu Hassan aliibuka mshindi kwa kupata kura milioni 31.9 milioni kati ya kura 37.8 zilizopigwa, sawa na asilimia 97.6 ya kura zilizopigwa siku hiyo, huyaoni kwenye tovuti za vyombo vya habari vya Tanzania.
Ukitumia tovuti za utafutaji (Search Engine) utakutana na matokeo hayo ya Rais katika tovuti na mitandao ya kijamii ya vyombo vya habari vya kimataifa na vya kikanda hususan nchi za Kenya, Uganda, Afrika Kusini na Ghana.
Matokeo ya ubunge na udiwani ndio kabisa huwezi kutana nayo katika mfumo wa umma (public domain) yawe ya mbunge au diwani mmoja mmoja au hata kimkoa, jambo ambalo wengi hatukulitarajia kwa uchaguzi uliotangazwa ndani ya saa 72.
Katika mazingira kama haya, binafsi nilitarajia tovuti ya INEC ya www.inec.go.tz ingekuwa imepakua (upload) matokeo hayo ambayo Watanzania tulio wengi tunatamani kufahamu namba za ushindi wa wabunge na madiwani wetu.
Leo hii si wanahabari, watafiti na waliokuwa wagombea imekuwa vigumu kupata matokeo hayo ili angalau basi kufanya ulinganisho wa idadi ya waliopiga kura uchaguzi mkuu 2025, na idadi ya waliojiandikisha uchaguzi mkuu wa 2020.
Nawapa mtihani, tafuteni matokeo ya ubunge na udiwani kwa majimbo na kata zote za Tanzania kama utayapata kirahisi, ni kwa sababu kuzimwa kwa intaneti kuliathiri urushaji, utangazaji na uchapishaji kwa vyombo binafsi vya habari.
Matokeo haya kwa sehemu kubwa yalikuwa yakirushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) na Chanel Ten na televisheni chache ambazo zilikuwa zikijiunga na matangazo mubashara ya TBC1.
INEC ndicho chombo cha kikatiba cha Tanzania Bara kwa mujibu wa Ibara ya 74 na Sheria ya INEC ya mwaka 2024 kilichokabidhiwa majukumu ya kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani hapa Tanzania.
Hatuna chombo kingine chochote hapa Tanzania, ambacho tutakinyooshea kidole kwa kukosa taarifa hizi muhimu kwa ustawi wa taifa letu zaidi ya INEC hasa ikizingatiwa Rais, wabunge na madiwani wote walishaapa kushika nyadhifa hizo.
Lakini leo ukiingia katika tovuti ya INEC, unakutana na kichwa cha habari “Matokeo ya kiti cha Rais na Makamu wa Rais uchaguzi mkuu 2025”, lakini kwa bahati mbaya sana ukigusa (click) yanakuja maneno “Hakuna taarifa kwa sasa”.
Mimi binafsi na pengine Watanzania tulio wengi, tunaona INEC inavunja Ibara ile ya 18(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.
Kwa faida ya wasomaji wa makala hii, Ibara hiyo ndogo inasomeka “Kila mtu anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii”.
Leo hii Januari 21,2026 tangu matokeo ya Rais yatangazwe Novemba 1,2025 na ya wabunge na madiwani kutangazwa ndani ya saa 48 kuanzia saa 10:00 ya Oktoba 29,2025 zimepita takribani siku 81, INEC haijapandisha (upload) matokeo hayo.
Matokeo ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani uliofanyika Oktoba 28,2020 unakutana nayo katika gazeti la Serikali (ISSN 0856-0323), Toleo Maalum lililoandikishwa Posta kama gazeti la Serikali na kuchapishwa Januari 5,2020.
Sasa kama INEC iliweza kutangaza matokeo ya urais ya uchaguzi mkuu 2025 ndani ya saa 72 tangu kukamilika upigaji kura na ya ubunge na udiwani ndani ya saa 48 licha ya kutokuwepo intaneti, wanashindwa nini kuyaweka katika tovuti?.
Kama matokeo ya Rais yalitangazwa na akaapishwa na kwenye vyombo vingi vya habari vya nje na vichache vya Tanzania unakutana nayo, kwani INEC isione ina wajibu wa kikatiba wa kuuhabarisha umma wa Watanzania matokeo yote?
Binafsi hivi sasa ni mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) na utafiti wangu naufanya katika eneo la uchaguzi, lakini hupati rejea za matokeo ya uchaguzi mkuu 2025.
Mwaka 2021, Wenzetu Nigeria kupitia Tume yao Huru ya Taifa ya Uchaguzi walikuwa wanaandika sheria ambayo wanaamini itawawezesha kusambaza matokeo ya uchaguzi kielektroniki au kidijitali kwa mafanikio kama ilivyo Kenya.
Katika uchaguzi mkuu wa 2022, Tume ya Uchaguzi na Mipaka ya Kenya (IEBC) walikuwa na kitu kinaitwa IEBC results Portal 2022 ambapo umma unaweza kuona matokeo kadri yanavyopokelewa kutoka vituo mbalimbali tena kwa wakati sahihi.
Nchi zingine zenye mfumo kama huo ni Afrika Kusini, Namibia, Liberia na Benin.
Bahati nzuri ripoti ya kikosi kazi kilichoundwa na Rais Samia chini ya Mwenyekiti wake, Profesa Rwekaza Mukandala kilipendekeza matumizi ya Tehama katika mchakato wa uchaguzi kwamba yahamasishwe na kiwango chake kiongezwe.
Katika ripoti hiyo ambayo ilikabidhiwa kwa Rais Samia Oktoba 21, 2022, kikosi hicho kilipendekeza pia zitayarishwe kanuni mahsusi za kuratibu matumizi ya Tehama kwenye mchakato wa uchaguzi na kuwepo na uwekezaji wa kutosha kwenye miundombinu ya Tehama na usalama wake wakati wa uchaguzi.
Tangu kikosi hicho kitoe mapendekezo yake, zimeshapita siku 1,188 na bado tuko zama zile zile za kabla ya mapendekezo kiasi kwamba hadi leo umma hauwezi kufikia (access) matokeo ya ubunge na udiwani kwenye tovuti ya INEC.
Binafsi siwalazimishi mpandishe matokeo hayo ila najaribu kuonyesha namna gani mnapopandisha matokeo kwa wakati mnaongeza uwazi na kuondoa minong’ono inayoweza kujitokeza kutokana na kuchelewesha.
Ni haki ya kikatiba ya wananchi kupata taarifa hizo kwa wakati hasa ikizingatiwa kuwa matokeo katika vituo vya kupigia kura 99,895 (kwa mujibu wa tovuti ya INEC) yalipokelewa kwa wakati na matokeo yakatangazwa ndani ya saa 72.
Nini kinakwamisha kupakiwa kwa matokeo ya uchaguzi mkuu 2025?. Hizi ni zama za tekinolojia, kama namba tayari mnazo tangu siku 81 zilizopita, kwa nini hampandishi matokeo hasa ikizingatiwa umma ulikuwa gizani Oktoba 29.
Mnaweza kusema TBC1 na ZBC zilikuwa zinatangaza, lakini kwa sisi watafiti tunapataje rejea? Leo hii ukimuuliza mwananchi wa kawaida katika jimboni kwake anaweza asijue mbunge wake au diwani alipata kura ngapi. Si sawa.
Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.
Anapatikana kwenye namba 0656600900