Venezuela. Kamandi ya Kusini ya Jeshi la Marekani (Southcom) imeikamata meli ya mafuta inayomilikiwa na Venezuela kwenye Bahari ya Caribbean, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na jeshi hilo jana Jumanne Januari 20, 2026.
Vikosi hivyo vimesema meli hiyo ya Sagitta, ilikuwa imekiuka marufuku iliyowekwa na Rais Donald Trump. Ukamataji huo unakuja ikiwa ni karibu siku 20 zimepita tangu kukamatwa kwa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Nicolas Maduro.
Januari 3, 2026, Jeshi la Marekani lilimkamata Maduro na sasa anakabiliwa na mashtaka kwenye mahakama ya New York.
Kupitia mtandao wa X, kamandi hiyo imesema: “Marekani imejitolea kuhakikisha kuwa mafuta pekee yanayoondoka Venezuela ni yale yanayopitia njia halali za kisheria.”
Kukamatwa kwa meli hiyo ni sehemu ya operesheni za wiki za hivi karibuni, baada ya Trump kutangaza kile alichokiita “marufuku kamili ya meli zote za mafuta kuingia na kutoka Venezuela”.
Trump analishutumu taifa hilo la Amerika Kusini kwa kuiba mafuta, ardhi na mali nyingine za Marekani na amesema lazima mali hizo zirejeshwe.
Aidha, hatua hiyo inatajwa kama sehemu ya jitihada za kukabiliana na shughuli haramu.