Kijana mbaroni kwa tuhuma za mauaji, uporaji wa pikipiki na fedha

Mbeya. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mawazo Msangawale (24), mkazi wa Mlowo mkoani Songwe, kwa tuhuma za kumuua kijana Juveni Baraka (18), kwa kumkata na kitu chenye ncha kali kichwani.

Mbali na kutekeleza mauaji hayo, alifanikiwa kutoweka na pikipiki aliyokuwa akitumia marehemu na   Sh1.5 milioni alizokuwa nazo marehemu kwa ajili ya kununua madini ya dhahabu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo leo Jumatano Januari  21, 2026 huku chanzo kikitajwa kuwa ni tamaa ya kujipatia fedha na mali.

Kuzaga amesema tukio la mauaji hayo lilitokea Januari 9, 2026 ambapo mwili wa marehemu ulipatikana Januari 10, 2026 ukiwa umetelekezwa porini.

“Kufuatia tukio hilo, Polisi kupitia askari wa kuchunguza matukio ya mauaji, walianza msako mkali ambapo Januari 15, 2026 walifanikiwa kumkata mtuhumiwa eneo la Mpemba, mji mdogo wa Tunduma mkoani Songwe,” amesema.

Kuzaga amesema mtuhumiwa alikamatwa saa 9 alasiri, akiwa na pikipiki iliyotumiwa na marehemu siku ya tukio.

Amesema uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hilo ni tamaa ya kujipatia fedha na mali kwa njia zisizo halali.

Kamanda Kuzaga amesema siku ya tukio mtuhumiwa alimpigia simu marehemu kumtaka amfuate kwenye pori lililopo Mto Mapogoro kwa lengo la kwenda kumuuzia madini ya dhahabu.

“Taarifa za awali zinaeleza baada ya marehemu kupata simu ya biashara ya madini ya dhahabu, aliwaaga wenzake na kuazima pikipiki, sambamba na kuchukua Sh1.5 milioni kwa ajili ya kununua madini hayo,” amesema.

Kuzaga amesema tangu siku ya tukio, marehemu hakuonekana tena hadi alipokutwa ameuawa kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali kichwani na mwili wake kutelekezwa porini.

Katika hatua nyingine, Kamanda Kuzaga ameionya jamii kuachana na tabia ya tamaa ya mali kwa njia zisizo halali na kukatisha uhai wa watu na ndoto zao.