Kipa Alliance ajivunia ubora, akiiwaza Simba

KIPA wa zamani wa Yanga Princess, Husna Mtunda ameanza vyema ndani ya kikosi cha Alliance Girls ya Mwanza akitoa mchango mkubwa kwa kuzuia nyavu za lango lake kuguswa na wapinzani.

Mtunda alijiunga na timu hiyo msimu huu akiwa mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba na Yanga Princess, akichukua nafasi ya Nusra Jafari aliyetimkia Fountain Gate Princess.

Akiwa na Alliance Girls msimu huu katika Ligi Kuu Wanawake, kipa huyo ameanza katika michezo yote tisa na kutoruhusu bao kwenye mechi tano, huku akifungwa mabao saba.

Kesho, Ijumaa, kipa huyo atakuwa na kibarua kizito mbele ya Simba Queens katika mchezo wa ligi utakaopigwa saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Alliance Girls imeshinda mechi sita kati ya tisa, sare moja na kupoteza mbili, huku ikipachika mabao saba na kuruhusu saba, ambapo imevuna alama 19 huku ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo nyuma ya vinara Simba Queens, Yanga Princess na JKT Queens.

Akizungumzia kiwango chake, Mtunda alisema uzoefu ambao ameupata kwenye ligi kwa takribani miaka saba sasa unamsaidia kufanya vizuri na kujifunza kila siku.

“Najisikia vizuri kuwa kwenye timu ya Alliance na kitu kinafanya najisikia furaha ni kucheza wakati wote kunazidi kuniimarisha,” alisema Mtunda na kuongeza:

“Alliance ni timu nzuri, ina wachezaji wazuri japokuwa wengi ni wachanga na hawana uzoefu wa mikikimikiki ya ligi, lakini wanapambana kuhakikisha tunatimiza lengo la klabu kumaliza nafasi nne za juu msimu huu.”

Ofisa Habari wa Alliance, Simon Kabwema, alisema; “Uwepo wake kwenye kikosi umeongeza utulivu sehemu ya ulinzi kwasababu anajua ni wakati gani timu ifanye kitu hiki, kwahiyo amekuwa kiongozi uwanjani, msimu uliopita tulikosa kiongozi.”

Akizungumzia mchezo dhidi ya Simba Queens, Kabwema alisema awali waliliomba Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) mchezo huo upigwe jijini Dar es Salaam kwa kuwa walikuwa wametoka kucheza ugenini mkoani Lindi dhidi ya Ruangwa Queens, lakini ombi lao lilikataliwa hivyo imewalazimu kurudi Mwanza kujiandaa na mchezo huo.

“Tupo njiani tunarudi Mwanza kipaumbele chetu ni mchezo wa Simba kwa sasa, ndiyo maana hata suala la mazungumzo ya mkataba mpya na benchi la ufundi tumeyasimamisha kwanza. Tukirudi Mwanza baada ya mechi na Simba ndiyo mazungumzo rasmi yataenda kufanyika,” alisema Kabwema.