Kocha Yanga atia neno ishu ya Ahoua

TAARIFA za Simba kumuuza kiungo Jean Charles Ahoua, kwa namna moja zimeonekana kumshtua kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi raia wa Tunisia.

Simba imemuuza Ahoua kwenda CR Belouizdad ya Algeria, huku kiungo huyo akishindwa kuanza vyema msimu huu tofauti na uliopita ambao aliibuka kinara wa mabao Ligi Kuu Bara akifunga 16.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa Ubelgiji, Nabi amesema ameshtushwa na taarifa za Ahoua kuondoka Simba, akiamini kutokana na kile kinachoendelea ndani ya klabu hiyo, alipaswa kuendelea kubaki.

Nabi amesema wakati akiwa Kaizer Chiefs, aliwahi kuvutiwa na Ahoua na hatua ya kumsajili ilikwama kutokana na mkataba wake na Simba, akiwa amebakiza mwaka mmoja wakati huo.

AHOU 01


“Nimeshtushwa sana, sikutarajia kama wangemwachia kwa haraka hivi. Ahoua si mchezaji mwenye mambo mengi, lakini akiwa uwanjani ana akili kubwa sana na utulivu. Unahitaji kutulia kujua ubora wake.

“Nilipokuja Tanzania niliona ubora wake. Wakati huo nilikuta ana akili ya kutaka kuwa mfungaji bora. Kama ningebaki Kaizer Chiefs, nilikuwa namhitaji sana nimsajili,” amesema Nabi aliyeifikisha Yanga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu wa 2022-2023.

AHOU 02


Aidha, Nabi amesema Simba haikutakiwa kumuachia mchezaji aliyefanya makubwa msimu wake wa kwanza kwa kuwa mfungaji bora, kwani Wekundu hao walikuwa bado wanaendelea kujenga timu yao, hivyo kubakisha wachezaji bora lilikuwa suala muhimu.

“Haikuwa nzuri sana kuuza mchezaji wako bora ambaye msimu wake wa kwanza amekupa thamani kubwa. Simba bado wanatengeneza timu yao, wanatakiwa kutunza wachezaji wao bora.

Ahoua ameondoka Simba akiacha rekodi ya kufunga mabao 17 katika Ligi Kuu Bara akicheza kwa msimu mmoja na nusu. Msimu wa kwanza 2024-2025 alifunga 16 na msimu huu 2025-2026 analo moja.