Marekebisho hati ya mashtaka kesi ya kughushi mafuta moto

Mabadiliko ya hati ya mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi inayotokana na mashtaka ya kujipatia kwa njia za udanganyifu  shehena ya mafuta yenye thamani ya zaidi ya Sh10 bilioni yameibua mvutano mkali wa hoja za kisheria baina ya mawakili a pande mbili.

Kutokana na mvutano huo kesi hiyo imekwama kuendelea kusikilizwa na mwenendo kabidhi, kwa ajili ya uhamishaji kesi hiyo kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam, Kisutu, inayosikiliza kesi hiyo katika hatua ya uchunguzi wa awali.

Badala yake mahakama hiyo imelazimika kuahirisha usikilizwaji wa mwenendo kabidhi huo mpaka Januari 26, 2026 kwa ajili ya uamuzi wa hoja hizo.

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Joseph Matage; Grace Matage ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya RHG General Traders Ltd na pia ni wakala wa forodha; Jamal  Saad, Mubinkhan Dalwai, Stanley Tibihenda, Edward Omeno na Bushira Ally, wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5195 ya mwaka 2025, washtakiwa hao wanakabiliwa na jumla ya mashtaka 13, ambayo ni pamoja na shtaka moja la kuongoza genge la uhalifu na mashtaka matano ni ya kughushi nyaraka.

Mengine ni mashtaka matano ya kuwasilisha nyaraka za uongo katika Bandari ya Dar es Salaam, shtaka moja la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na shtaka moja la utakatishaji fedha.

Hata hivyo, washtakiwa wote wapo rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili halina dhamana.

Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka hayo Februari 28, 2025 kwa ajili ya uchunuzi wa awali ikiwemo ukamilishaji upelelezi, kabla ya kesi hiyo kuhamishiwa Mahakama Kuu ambayo ndiye yenye mamlaka ya kuisikiliza.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Gwantwa katika hatua hiyo ilipangwa leo Jumatano, Januari 21, 2026 kwa ajili ya mwenendo kabidhi, ambapo washtakiwa wangesomewa maelezo ya mashahidi wa Jamhuri wanaotarajiwa kuitwa pamoja na vielelezo vitakavyotumika, kisha mahakama kutoa amri ya kuihamishia Mahakama Kuu.

Kabla ya hatua hiyo Jamhuri imeomba kwanza kufanya marekebisho ya ya hati ya mashitaka kwa kumuongeza mshitakiwa wa nane ambaye ni kampuni ya Matage Traders and Logistic Company Limited.

Wakili wa Serikali, Hellen Masululu akishirikiana na Wakili Pancransia Protas ameomba kufanya mabadiliko hayo ya hati ya mashtaka chini ya kifungu cha 251 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA).

Amedai kuna mshitakiwa namba nane ambaye ni kampuni tajwa anatakiwa kuongezwa katika hati ya kabla ya kuendelea na hatua hiyo ya mwenendo wa kabidhi.

Hata hivyo, wakili wa utetezi, Peter Madeleka anayemwakilisha mshtakiwa wa tatu, Saad, amepinga ombi hilo la Jamhuri.

Wakili Madeleka amedai kuwa kifungu cha 251 cha CPA kilichorejewa na wakili wa Serikali kinaeleza kuwa marekebisho hayo yanaweza kufanyika katika hatua ya usikilizwaji kwenye mahakama yenye mamlaka ya usikilizaji kesi husika na si katika Mahakama ya Ukabidhi.

Wakili Madeleka amedai kuwa kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo kwa kuwa ni Mahakama ya Ukabishiid na si mahakama yenye mamkala ya usikilizaji, basi haina mamlaka ya kusikiliza ombi hilo na akaiomba ilitupilie mbali ombi hilo la Jamhuri.

“Kwa kuwasaidia ili waweze (Jamhuri) kufanya hivyo (kurekebisha hati ya mashtaka) wanatakiwa wa-enter nolle prosqui (wayaondoe mashtaka) chini ya kifungu cha 92(1) cha CPA alafu wawashitaki tena ili waweze kumuongeza mshitakiwa wanayetaka kumuongeza au waondoe kesi mahakamani ili waandae hati mpya ili kumuongeza mshitakiwa,” amedai Madeleka.

Akijibu hoja hiyo, Wakili Masululu amepinga hoja za wakili Madeleka akidai kuwa lengo la mwenendo kabidhi ni kujua tu kuna mashahidi mangapi na ushahidi utakao tumika wakati wa usikilizwaji, hivyo bila kuongeza mshitakiwa huyo mbeleni itaonekana kuwa mshitakiwa huyo hajatendewa haki.

Amesisitiza lengo la kumjumuisha mshtakiwa huyo kabla ya mwenendo kabidhi ni kuwezesha mshtakiwa huyo mpya wanayekusudia kumuongeza kukabidhiwa (Mahakama Kuu) kwa pamoja na wengine na kwamba wanaaona kuwa kifungu wezeshi walichokirejea ni kifungu sahihi kabisa.

Kwa upande wake, wakili Pancransia ameunga mkono hoja za wakili Masululu, huku akiweka uzito katika hoja hiyo kwa kuielekeza Mahakama katika uamuzi wa Mahakama Kuu kwenye moja ya kesi ilizokuwahi kuziamua kuhusu hoja hiyo bishaniwa.

Amedai katika kesi hiyo Mahakama Kuu ilieleza kuwa mahakama ya chini ina mamlaka ya kuamuru kama mshitakiwa yupo magereza apelekwe au kama hajakamatwa akamatwe ili asomewe hati na taarifa.

Hivyo ameiomba mahakama ikubali ombi lao ili mshitakiwa huyo mpya aingizwe kwenye hati ya mashtaka, asomewe mashtaka hayo kisha ahusishwe kwenye mwenendo kabidhi huo, akidai kuwa tayari yupo mahakamani.

Hata hivyo, wakili Madeleka amesisitiza hoja zake za awali na kuomba mahakama isikubali ombi hilo.

Hakimu Mwankuga baada ya kusikiliza hoja za pande zote amesema kuwa mahakama inatakiwa kuandaa uamuzi kujibu swali la iwapo katika hatua hiyo Jamhuri inaweza kuomba mahakama kufanya marerkebisho ya hati ya mashitaka au la, huku akipanga kutoa uamuzi huo Januari 26.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka ya sasa washakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Juni Mosi na Novemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam na maeneo mengine, kwa nia ovu, waliandaa genge la uhalifu.

Wanadaiwa kuandaa genge hilo la uhalifu kwa lengo la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambazo ni dola za Marekani 4,627,459.14 sawa na zaidi ya fedha za Kitanzania zaidi ya Sh11.3 bilioni.

Pia wanadaiwa kuwa kwa nyakati tofautitofauti zikiwemo kati ya Julai Mosi na Agosti 12, 2024 jijini Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu, walioghushi nyaraka za uongo iitwayo Delivery Order ikiwemo yenye kumbukumbu namba APU 04638 ya Agosti 12, 2024.

 Wanadaiwa kuwa walighushi nyaraka hizo kwa lengo la kuonyesha kuwa ni halali na imetolewa na kampuni ya Nyota Tanzania Ltd, kupitia wakala wa meli Maersk Group, wakati wakijua kuwa nyaraka hizo ni za uongo.

Vilevile wanadaiwa kuwa kwa nyakati tofauti ikiwamo Agosti 12, 2024 kwa njia ya udanganyifu waliwasilisha nyaraka za uwongo katika Bandari ya Dar es Salaam.

Wanadaiwa waliwasilisha nyaraka hizo za uwongo  kwa lengo la kuonyesha kuwa ni halali na imetolewa na kampuni ya Nyota Tanzania Ltd kupitia wakala wa meli Maersk Group, wakati wakijua kuwa ni uongo.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa kuwa kati ya Juni Mosi na Novemba 30, 2024 jijini Dar es Salaam, kwa njia ya udanganyifu walijipatia kilo 6,367,262 za mafuta ya kupikia aina Camar zenye thamani ya dola za Marekani 4,627,459 (zaidi ya Sh11.3 bilioni).

Ilielezwa kuwa walijipatia mafuta hayo mali ya kampuni ya AAstar Trading PTE Ltd kwa kudanganya kwamba bili halisi ya shehena ya mafuta hayo ilitolewa na kampuni ya Nyota Tanzania Ltd kupitia Maersk Group, wakati wakijua kuwa ni uongo.

Vilevile wanadaiwa kuwa kati ya Juni Mosi na Novemba 30, 2024, kwa pamoja walijihusisha na miamala ya fedha yenye thamani ya dola za Marekani 4,627,459.

Wanadaiwa kuziweka fedha hizo kwenye akaunti ilizofunguliwa katika benki ya Equity yenye jina la Makange Logistics and Traders Company Limited, wakati wakifahamu kuwa miamala hiyo ni mazalia ya kosa tangulizi la kughushi nyaraka.