Mchungaji wa EAGT akutwa amefariki chumbani Moshi

Moshi. Mchungani wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Makimbilio, Manispaa ya Moshi, Jane Mwangalimi, amekutwa amefariki dunia nyumbani kwake alikokuwa akiishi na mjukuu wake wa miaka mitano.

Tukio hilo limetokea Januari 20, 2026 limegunduliwa na mjukuu wake huyo aliyekuwa akiishi naye, mtaa wa Kariwa Chini, Kata ya Rau, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro baada ya kumuamsha bibi yake asubuhi kwa muda mrefu bila kuamka wakati alipohisi njaa.

Tukio hilo la mtu kukutwa amefia ndani limetokea ikiwa ni siku tano baada ya kutokea kwa tukio linalofanana na hilo ambapo Deogratius Ottaru (39) mkazi wa kitongoji cha kidachini kata ya kibosho Kirima, alikutwa amekufa chumbani kwake.

Akilizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro,  Simon Maigwa amesema baada ya kupata taarifa walifika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu ambao umehifadhiwa hospitali ya KCMC kwa uchunguzi wa kitabu.

“Uchunguzi utafanyika kubaini chanzo cha kifo ili kuondoa mashaka kwa jamii,” amesema Kamanda Maigwa

 

Jirani asimulia mjukuu alivyobaini kifo cha bibi yake

Akielezea namna mtoto huyo alivyobaini kifo cha bibi yake, mmoja wa majirani wa Mchungaji huyo, Calista Lyimo amesema mtoto huyo baada ya asubuhi kukucha na kuona bibi yake haamki alimgusa gusa lakini hakujigusa jambo lililompa wasiwasi.

Amesema, alimsogelea bibi yake huyo na kumtazama usoni, ndipo alipoona akitokwa na damu mdomoni, hali hiyo ilimfanya atumie kiti kupanda juu ya mlango na ndipo alipofanikiwa kufikia kitasa cha mlango na kufanikiwa kufungua mlango na kutoka nje.
Amedai baada ya kufungua mlango na kutoka nje alikwenda kutoa taarifa kwa majirani kwamba bibi yake haongei na hajigusi, ambapo mmoja wa majirani alifika nyumbani hapo na kisha taarifa kutolewa kituo cha polisi.

Mwili wa Mchungaji, Jane Mwangalimi(EAGT), ukitolewa ndani ya nyumba yake. Picha na Jesse Tunuka



Aidha, amesema tukio hilo limemshtua zaidi kwa kuwa usiku wa kuamkia Januari 20 walikuwa pamoja katika ibada ya maombi ya jioni.
“Tulifanya maombi nyumbani kwangu hadi saa mbili usiku. Baada ya hapo aliniambia anajisikia vibaya kidogo, nikamwambia labda ni uchovu, sikujua kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wa kumuona akiwa hai,” amesema jirani huyo.

Akisimulia tukio hilo kwa sauti ya upole, David Chuwa ambaye ni mjukuu wa mchungaji huyo, amesema aliamka asubuhi akimwita bibi yake aamke amuandalie chakula, lakini hakuzungumza.
“Nilimwita bibi anipikie, nikamwita tena, hakusema chochote,” amesema David.
Mtoto huyo amesema alipomkaribia zaidi bibi yake akiwa kitandani, aliona hali isiyo ya kawaida.“Nilimkuta amelala tu, alikuwa anatokwa damu nyeusi mdomoni, nilimwita tena lakini hakuitika,”
Mtoto huyo amesema, kwa njaa aliyokuwa nayo na hofu iliyomkumba vilimfanya atafute msaada nje ya nyumba, licha ya mlango kuwa umefungwa.

“Nilikua na njaa sana. Nikajaribu kufungua mlango nikashindwa, nikapanda juu ya viti nikafikia kitasa nikafungua nikatoka nje,” amesema.

Amesema, baada ya kufungua mlango, alitoka nje na kuwatafuta watu wazima waliokuwa karibu.“Nikatoka nikamwambia Aines, mama Amu na mama Queen. Niliwaambia bibi haamki na anatokwa na damu mdomoni,” amesema mtoto huyo.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Mtaa wa Kariwa Chini, Thomas Materu, amesema baada ya kupata taarifa kupitia balozi wa eneo hilo, alifika eneo la tukio na alipothibitisha ni kweli mama huyo amefariki aliwasiliana na vyombo vya ulinzi na usalama.

Naye, mmoja wa viongozi wa Kanisa hilo, Calvin Lyimo, amesema Mchungaji huyo alikuwa akisumbuliwa na changamoto za kiafya ikiwemo kizunguzungu na matatizo ya kuganda kwa damu.

“Alikuwa mama wa kiroho kwangu, na alikuwa akinieleza changamoto zake za kiafya maana alinilea kiimani na mchango wake hauwezi kusahaulika kwangu,” amesema kiongozi huyo.

 

Mwanasaikolojia asisitiza umuhimu wa kupima afya

Akizungumzia masuala ya watu kufa vifo vya ghafla, mwanasaikolojia, Godfrey Mbowe amesema changamoto kubwa inayojitokeza ni kwamba baadhi ya watu hutembea na msongo wa mawazo kwa muda mrefu hali ambayo hupelekea changamoto hiyo.

“Watu hutembea na shinikizo la damu la juu kubwa bila kujua na hii inasababishwa sana na msongo wa mawazo wa muda mrefu au mtu anapita kwenye adha fulani kubwa kwenye maisha yake, na hajaweza kutanzua hiyo shida kwa hiyo unakuta anatembea na shinikizo la damu kwa muda mrefu na tukio la kufa ghafla linaweza kutokea,”amesema Mbowe.