Mikopo ya halmashauri pasua kichwa Mtama

Mtama. Madiwani wa Halmashauri ya Mtama wamelalamika kwenye baraza la madiwani kuwa katika maeneo yao kuna baadhi ya wananchi ambao wamepewa fedha pungufu tofauti na kiasi cha mikopo waliyoidhinishiwa na halmashauri .

Akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani cha robo ya pili, leo Jumatano Januari 21,2026 Diwani Viti maalumu kata ya Pangatena,  Hawa Nameta amesema kuna baadhi ya vikundi vimemlalamikia kuwa wamepewa mkopo wa Sh1.5 milioni huku deni lao likisoma Sh3 milioni.

Kufuatia hilo diwani huyo ameitaka halmashauri kufuatilia kwa umakini mikopo wanayoitoa ili kupunguza changamoto ya ulipaji wa madeni.

“Kata yangu kuna kikundi cha walemavu watatu, walikuja kunilalamikia kwamba waliomba mkopo wa halmashauri waliidhinishiwa Sh3 milioni, kwa maana ya Sh1 milioni kwa kila mmoja  ,lakini wamepewa Sh1.5 milioni na deni linasoma Sh3 milioni”amesema Nameta.

Pia amesema kwa aina hiyo wakopaji hawataweza kurejesha Sh3 milioni wakati wamepewa Sh1.5 milioni na kuitaka Serikali ifuatilie kwa umakini fedha hizo za mikopo.

Baadhi ya madiwani wakichangia hoja kwenye baraza la madiwani robo ya pili katika Halmshauri ya Mtama.



Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,  Yusuph Tipu pamoja na baraza lake wameiagiza watendaji kufuatilia kwa kina vikundi hewa na vilivyopokea fedha isiyoendana na iliyoidhinishwa.
Katibu Tawala Wilaya ya Lindi, Udhaifa Rashidi ambaye pia ni mjumbe wa uhakiki wa mikopo ngazi ya Wilaya ameliambia baraza kuwa mwaka jana walipitisha vikundi vya walemavu kwa asilimia 90.

“Mwaka jana tulipitisha vikundi vingi vikiwemo vya walemavu tulipitisha asilimia 90, niliwataka wanavikundi kama itatokea mtendaji wa idara ya utoaji mikopo ataomba fedha kama hisani watoe taarifa lakini kwa bahati mbaya hakuna aliyetoa taarifa, wanalalamika pembeni niwaombe madiwani kutuletea ushahidi ili tuweze kulifanyia kazi jambo hili.”amesema Rashidi.

Naye ofisa maendeleo ya jamii wa halmashauri hiyo, Patricia Peter amesema kuwa jumla ya madeni yote ni Sh466 milioni kati ya hizo Sh292 milioni ni madeni yaliyomo ndani ya muda na madeni ambayo yamemaliza muda wake bado hayajarejesha ni Sh173 milioni.