Mkurugenzi wa halmashauri Mbeya aagiza wagonjwa kutibiwa kabla ya malipo

Mbeya. Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Mkoa wa Mbeya, imeweka msisitizo kwa Hospitali za Serikali wilayani humo, kuhudumia wagonjwa kabla ya malipo ili kuokoa maisha na  kupunguza malalamiko.

Hatua hiyo imetajwa ni kutekeleza maagizo ya Serikali katika kusimamia sera ya afya kwa vitendo kwa lengo la kuwezesha Watanzania kunufaika kwa kuboreshwa upatikanaji wa huduma za matibabu kwa wakati pasipo vikwazo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mbarali Mkoa wa Mbeya, Raymond Mweli ameliambia Mwananchi leo Jumatano Januari 21, 2026, wakati akizungumzia mikakati ya  kuboresha upatikanaji wa huduma muhimu kwa jamii.

“Hilo halina mjadala mikakati yetu kama halmashauri  ni kuona  wananchi wanapofika kupata matibabu wahudumiwe kwanza ndipo  taratibu za malipo zifuate  lengo ni kuondoa malalamiko na  kuokoa maisha ya wagonjwa hususani wa dharura,” amesema.

Mweli amesema suala hilo lazima lipewe kipaumbele cha hali ya juu ambalo viongozi wakuu wa nchi wametolea maelekezo mara kadhaa akiwepo Rais Samia Suluhu Hassan lengo kuona Watanzania wanapata huduma bora za afya.

Mweli amesema katika kuhakikisha linatekelezwa kwa vitendo atafanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kujirishisha kuona jamii inanufaika na uwekezaji wa Serikali katika upatikanaji bora wa huduma za afya.

“Haitapendeza kusikia mgonjwa kafika kupata matibabu kakosa huduma kwa sababu hajalipa fedha dirishani katika hilo nikipata malalamiko sitoweza kulifumbia macho,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mweli amesisitiza watendaji wa Serikali kuwajibika kuwatumikia wananchi endapo kuna  changamoto wawasilishe ofisini kwake ili ziweze kutatuliwa.

Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Ray Salandi amesema wamepokea maelekezo ya Mkurugenzi na kwamba utekelezaji tayari ulianza licha ya kuwepo kwa changamoto ya wananchi wasio waaminifu kutoroka na malipo baada ya kupata matibabu.

“Suala la matibabu kabla ya malipo  tunasimamia vyema hususani kwa wagonjwa wa dharura wakiwepo kina mama wajawazito, ajali, magonjwa sugu na watoto ikiwa ni kutekeleza maelekezo ya Serikali yenye lengo la kufikisha huduma bora za afya kwa jamii,” amesema.

Kuhusu changamoto ya wagonjwa kukimbia na fedha za malipo baada ya huduma.

Amesema kuna utaratibu wa kuwapata kwa kutumia maofisa maendeleo ya jamii eneo husika kwa kuzingatia taarifa za mgonjwa husika ambao wapo ambao tunawabaini.

“Kimsingi tunashukuru Mkurugenzi wetu kwa kuweka mkazo suala hilo tutaendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa kuzingatia sera ya afya na maelekezo ya Serikali,” amesema.

Tabu Joel Mkazi wa Ubaruku wilayani humo, amesema mfumo wa matibabu kabla ya malipo utaokoa maisha ya wananchi walio wengi kutokana na magonjwa ya dharura kama kuhara, maralia na magonjwa ya watoto.

“Tunashukuru hatua ya Serikali kusisitiza mfumo huu, kimsingi kuna baadhi ya wananchi wanakwama kwenda kupata huduma kutokana na kukosa fedha kwa wakati na kuugulia majumbani jambo ambalo pasipo kujua kuitwisha mzigo wa lawama Serikali,” amesema.