Wahenga walisema “Utavuna ulichopanda”. Kama ulipanda mahindi haiwezekani kuvuna mtama hata kama zote ni nafaka. Usemi huu una maana kubwa zaidi na kufanana na “Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo”. Malezi ya mtoto yanafananishwa na mbegu iliyopandwa na kuhudumiwa ikiwa ardhini. Ikiwa mbegu ni bora na imepandwa kwenye ardhi yenye rutuba, ni lazima itatoa mazao yanayotarajiwa.
Siku zote mipango ndiyo inayoamua matokeo. Mipango mizuri inaweza kuleta matokeo mazuri kiasi cha kusawazisha mabaya yaliyowahi kutokea. Lakini mipango ikiwa mibovu inaweza kuchanganya watu na kuamsha hasira hata zisizo na sababu. Ni sawa na kupanda mbegu ya ngano ikaja kuota mbigiri. Mkulima hataelewa, na jambo hili linaweza kumpelekea kuhisi kuwa anachezewa michezo ya kishirikina na wenzake.
Nchi yetu ilikuwa na mipango thabiti juu ya vijana wake katika siku zilizopita. Kijana aliandaliwa tangu akiwa shuleni, na hakuachwa mpaka alipoingia kwenye ajira. Tukawa na Taifa lenye nidhamu na uwajibikaji. Vijana wa nyakati zile walikuwa wazalendo kwa nchi na viongozi wao. Kila mwananchi alikuwa na wajibu wa kulinda na kujenga Taifa lake. Tulikuwa kama nyuki ambao hata wakiwa katika kundi kubwa, kila mmoja anajua wajibu wake.
Wakati ule hatukuathiriwa na maisha ya Kimagharibi. Tanzania ilikuwa ni nchi isiyofungamana na upande wowote. Ilikuwa na uhuru wa kuchagua marafiki bila kuingiliwa, na ilikuwa na mipango mizuri ya kuwajenga vijana wake kimaadili. Shule zote za Msingi zilikuwa na mashamba au bustani za wanafunzi.
Wanafunzi walihudumia mashamba kwa mtindo wa kilimo cha umwagiliaji hadi walipovuna. Haikujalisha maji yalichukuliwa umbali gani kutoka shuleni.
Unaweza kuona jinsi wakati huo tulivyokuwa mbele kimawazo. Lakini kwa bahati mbaya waliachwa ghafla njiani, shule zikabadilisha mashamba kuwa majengo.
Watoto hawa wajiojifunza kilimo cha umwagiliaji walikwenda na mafunzo yao nyumbani. Hatujui kama kiliwasaidia kwa kuwa bila shaka hakikupata mwendelezo. Sasa baada ya miongo mingi ndio tunasikia maandalizi ya skimu za umwagiliaji.
Wengine wanadhani watoto kuachishwa kujitegemea ilikuwa ni njia ya kuwasaidia. Lakini mimi sioni hivyo kwa sababu kama aliweza kusaidiwa hilo, ni kivipi akaachwa ahangaike na vyeti mkononi baada ya kuhitimu. Inasemwa kuwa teke la kuku halimuumizi kifaranga wake, nami nikiwa mmoja kati ya wanafunzi tuliopitia hayo tulishuhudia jinsi tulivyowajibika kwa furaha na vicheko shambani.
Dira ya Taifa ya wakati ule ingeendana na maisha ya Mtanzania, hivi sasa tungekuwa na wataalamu wengi wa kilimo. Ni mpango mzuri ambao ungetuvusha kuondokana na tatizo la ajira. Zaidi ya hapo kulikuwa na utaratibu wa vijana kunolewa na Jeshi la Kujenga Taifa. Walitayarishwa kwa kilimo na ufundi, hivyo walihimili hali yoyote waliyokutana nayo wakielekea kwenye ajira. Bila shaka hawakuwahi kufikiria kuzurura na vyeti barabarani wakati wakisaka ajira.
Tunaposema vijana wanaotoka masomoni wapimwe kabla ya kuingizwa kwenye soko la ajira, tumaanishe hivyo. Kijana aliyefunzwa kuagiza mahitaji ya ofisi, alijifunza pia kutafuta masoko. Mara alipoajiriwa, alikutana na miezi mitatu au zaidi ya majaribio kazini. Hapa ndipo mwajiri alipothibitisha kuwa kijana alikuwa na utayari wa kulijenga Taifa. Hakuweza kufeli kwenye changamoto za kazi zilizomhusu.
Hivi leo kijana asiye mzalendo anapoingia kwenye ajira, anafikiria mambo yake binafsi. Kwa kuwa aliondolewa kwenye stadi za kazi tangu shuleni na hajapitishwa kwenye uzalendo wa JKT, anaweza kuamua vyovyote pale anapowekwa kwenye usimamizi wa jambo fulani. Atafuata yale tu anayoyaona kwenye mitandao na kufuata njia ya vijana wenzake wa ulimwenguni. Tunawaona watumishi wa umma wa leo wasivyo na ubunifu wa kulisaidia Taifa.
Mifano ipo mingi, lakini kwa haraka ule usiofutika mapema ni hekaheka za bonde la Mto Msimbazi. Watu waligawiwa viwanja bila kujali historia ya eneo hilo kufurika kila baada ya muda fulani. Watendaji walijua maji yakishapata njia yake, huweza kutoonekana wakati wote wa kiangazi lakini wakati wa mvua ukifika, yatarudi palepale hata baada ya miongo mingi. Wangelikuwa wazalendo, wangebuni matumizi ya muda mfupi-mfupi wa maeneo hayo badala ya kuyafanya makazi.
Hili pia tunaliona katika baadhi ya Mikoa. Historia za mafuriko zimekuwa zikijirudia katika baadhi ya maeneo huku viongozi wakikosa ubunifu. Pamoja na mabadiliko ya hali ya nchi, Serikali iwekeze maeneo ya makazi kwa kuzingatia ushauri wa wanajiografia. Katika hali ya kawaida, mafuriko hayawezi kuvamia milima. Hakujawahi kutokea madhara ya mabadiliko ya hali ya nchi kwenye milima, lakini inawezekana kwa mabondeni kwa sababu za maumbile ya maji.
Moja ya njia za kurudisha nchi kwenye ubora wake ni kurudisha uzalendo. Hakuna anayeweza kuwadanganya wengine kwamba uzalendo hauna maana. Tunaona hivi sasa nchi za kibepari kama Marekani zikipigania uzalendo wa nchi zao, na zile za kijamaa kama China zikiimarisha hali hiyo.
Hakuna hata mmoja aliyewahi kudhani kuwa wababe wa uchumi kama Wamarekani, wangewahi kutishwa na maendeleo ya nchi masikini kama China. Siri kubwa ni Wachina kushikilia dira yao tangu enzi za Mao, hadi ujamaa na uzalendo kuwafikisha hapa walipo leo.