Dodoma. Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Marekani wametangaza mpango wa utafiti wa kina wa madini ya kinywe hatua inayolenga kuongeza tija ya rasilimali za madini, kufungua fursa za ajira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.
Akizungumza leo Jumatano Januari 21, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa Serikali ili kuhakikisha madini yanayotajwa kuwa na thamani kubwa duniani yanatambulika kikamilifu.
Mavunde amesema madini hayo ni muhimu kuhakikisha yanachimbwa kwa tija na kunufaisha moja kwa moja Taifa na wananchi.
Waziri Mavunde amesema utafiti wa awali umeonesha uwepo wa madini ya kinywe katika mikoa miwili ya Lindi na Mtwara, huku Serikali ikipanga kupanua wigo wa utafiti ili kupata takwimu sahihi za kijiolojia zitakazowezesha uwekezaji wenye tija na uchimbaji endelevu.
Waziri amesema Watanzania wanaomiliki leseni za uchimbaji wa madini watapewa kipaumbele katika mpango huo, hatua itakayowezesha wazawa kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini ili kuongeza kipato na kukuza uchumi wa ndani.
“Upanuzi wa utafiti unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa madini ya kinywe kwa siku zijazo, ambapo makadirio yanaonesha ifikapo mwaka 2050, Tanzania itaweza kuzalisha kiwango kikubwa cha madini hayo, hivyo kuongeza mapato ya Serikali na fedha kwa ajili ya huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya na miundombinu,” amesema Mavunde.
Mavunde ameishukuru Serikali ya Marekani kupitia Wizara ya Nishati na Madini kwa kuendeleza ushirikiano wa kitaalamu, ikiwemo kusaidia mafunzo kwa wataalamu wa ndani ili kujenga uwezo wa kitaifa katika sekta ya madini.
Mavunde amesema Watanzania watanufaika na mafunzo ya siku mbili ya kuchambua na kutafsiri takwimu za kijiolojia (Geo Data), yatakayoongeza ujuzi, ajira na ushiriki wa wazawa katika shughuli za madini.
Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Andy Lentz, amesema nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika miradi ya maendeleo, akisisitiza ushirikiano wa utafiti wa madini ya kinywe utakuwa wa muda mrefu na wenye manufaa kwa pande zote.