TANZANIA NA MAREKANI KUANZA MRADI MKUBWA WA UTAFITI WA KINA WA MADINI

………………..

Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Madini na Nishati ya Marekani imeandaa utekelezaji wa mradi mkubwa wa utafiti wa kina wa madini, unaolenga kuimarisha agenda ya maendeleo ya sekta ya madini nchini.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Antony Peter Mavunde   leo  21 Januari 2026 jijini Dodoma mbele ya waandishi wa habari    Mavunde amesema ushirikiano huo unalenga kuimarisha mahusiano ya kimkakati kati ya Tanzania na Marekani, pamoja na kujenga uwezo wa kitaalamu kwa Watanzania wanaofanya kazi katika sekta ya madini, hususan katika eneo la utafiti wa kina wa rasilimali za madini.

Pia Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizojaaliwa kuwa na rasilimali nyingi za madini ya aina mbalimbali, hali ambayo imeifanya nchi kuwa na nafasi muhimu katika kukidhi mahitaji ya madini yanayoongezeka duniani.

Aidha  Waziri Mavunde, ametaja  maeneo yenye leseni za madini yanayomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), ambapo kupitia ushirikiano huo, Tanzania na Marekani zitafanya utafiti wa pamoja ili kubaini maeneo yenye fursa kubwa za uwekezaji wa kimadini.

“Utafiti huu wa pamoja utatusaidia kubaini maeneo yenye utajiri mkubwa wa madini na kufungua fursa za uwekezaji, jambo litakalosaidia kuanzishwa kwa migodi mikubwa mipya, hususan katika mikoa ya Mtwara na Lindi,” amesema Mavunde 

Ameongeza kuwa Serikali ya Marekani imeonesha utayari wa kushirikiana na Tanzania katika kupanua maeneo ya utafiti wa madini pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa Kitanzania, ili kuwawezesha kusimamia ipasavyo rasilimali za madini kwa kutumia teknolojia za kisasa.

Waziri Mavunde amesema eneo linalotarajiwa kufanyiwa utafiti wa kina lina madini muhimu yanayojulikana kama madini kingwe (graphite), ambayo mahitaji yake duniani yanatarajiwa kufikia tani milioni 4.5 kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.

“Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kuwa miongoni mwa wasambazaji wakubwa wa madini ya graphite duniani kutokana na rasilimali tulizonazo,” amesema.

Ameeleza kuwa pamoja na utafiti wa madini, lakini pia kutakuwepo na mafunzo ya siku mbili ya kuwajengea uwezo wataalamu wetu hasa katika matumizi ya kisasa ya teknolojia ya hali ya juu ya kutafsiri takwimu za kimadini jodeita ambapo tunategemea watu wetu wa Tanzania kupitia vifaa hivi vitakavyokabidhiwa watakuwa na uwezo wa kutafsiri vizur  taarifa sahihi za utafiti katika eneo la madini.