Dar es Salaam. Mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump kuweka vikwazo vya kodi kwa Mataifa ya Ulaya umechukua sura mpya baada ya Umoja wa Ulaya (EU) kuchukua hatua za kulipiza kisasi.
Hatua za Trump zilizotangazwa Januari 2026, zinahusu ushuru wa ziada kwa bidhaa za viwandani kutoka Ulaya.
Akizungumza nchini Marekani, Rais Donald Trump alisema hatua hizo ni muhimu kwa kulinda uchumi wa taifa lake dhidi ya ushindani wa kimataifa kibiashara.
“Tumekuwa tukitendewa isivyo haki kwa muda mrefu. Ushuru huu ni wa kulinda wafanyakazi wetu, viwanda vyetu na mustakabali wa uchumi wa Marekani,” alisema Trump.
Kauli za Trump zilichochea taharuki barani Ulaya, hasa katika nchi zenye utegemezi mkubwa wa mauzo ya nje kama Ujerumani na Ufaransa.
Umoja wa Ulaya tayari umetangaza kuchukua hatua za kulipiza kisasi endapo Trump atatekeleza kikamilifu vitisho vyake vya ushuru wa kibiashara kwa bara hilo tajiri duniani.
Mataifa mengi ya Ulaya yakiwemo Ujerumani, Denmark na Ufaransa yametilia mkazo wa wazi kuhusu kulipiza kisasi kwa kutangaza ushuru mpya kwa bidhaa za Marekani barani Ulaya katika kukabili mpango huo wa Trump.
Wakati mpango huo ikitangazwa, Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent ameonya kuwa majibu ya aina hiyo kutoka Ulaya hayataisaidia dunia kiuchumi.
“Kulipiza kisasi hakutakuwa jambo la busara na kunaweza kuathiri vibaya uchumi wa dunia,” amesema Bessent.
Ujerumani imejitokeza hadharani kupinga vitisho hivyo vya ushuru vya Marekani, ikisema vinazidisha mzozo wa kibiashara na havikubaliki.
Katika taarifa ya Serikali ya Ujerumani, Berlin ilieleza iko tayari kuchukua hatua madhubuti kulinda maslahi ya kiuchumi ya taifa hilo na Umoja wa Ulaya.
“Tumeazimia kujibu kwa hatua madhubuti, ikiwa ni pamoja na ushuru wa kulipiza kisasi, na kuandaa sera zaidi za kiuchumi ikiwa italazimu,” amesema msemaji wa serikali ya Ujerumani.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa msimamo huo unaungwa mkono na nchi nyingi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
“Kuna makubaliano mapana miongoni mwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya, ni muhimu Umoja wa Ulaya uwe na msimamo wa pamoja,” imesema taarifa Ujerumani.
Pia, amesisitiza kuwa makampuni mapya na yenye mafanikio lazima yawe na mtaji wa kutosha na yaweze kukua ndani ya Umoja wa Ulaya.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Lars Klingbeil amesema Ujerumani na Ufaransa zinatafuta namna ya kuyaendeleza makampuni mapya yanayoendelea Ulaya ili kuimarisha uchumi wa bara hilo kama hatua ya kuondoa utegemezi wa bidhaa za Ujerumani.
Klingbeil, ambaye pia ni makamu wa kansela, amekiri bado Ulaya ina safari ndefu kufikia ushindani wa kimataifa unaohitajika, akitoa wito tushughulikia mapungufu ya ufadhili kwa makampuni yanayokua kwa kasi.
Kadri mvutano huo kibiashara unavyozidi kuongezeka, wachambuzi wanaonya vita vya ushuru vinaweza kudhoofisha uchumi wa dunia.
Hatua ya Ulaya kuibuka kwa mshikamano wa kisiasa na kiuchumi, ikijiandaa kukabiliana na shinikizo la Trump kwa umoja na sera madhubuti, inafanya dunia kusubiri Trump atachukua hatua gani kutokana na msimamo wake katika kutekeleza hatua ambazo amekuwa akichukua dhidi ya mataifa mbalimbali na kuzua mjadala wa kidiplomasia na kiuchumi.