Mbozi. Viongozi wote wa Serikali ya Kijiji cha Namwanga kilichopo katika Kata ya Hezya, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, wamejiuzulu nyadhifa zao, wakilalamikia vitendo vya ukandamizaji na udhalilishaji wanavyodai kufanyiwa na viongozi wa ngazi ya kata.
Viongozi hao, wakiongozwa na mwenyekiti wao, Japhet Mbukwa, walifikia uamuzi huo Januari 17, 2026, siku chache baada ya kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa amri ya Mtendaji wa Kata ya Hezya.
Akizungumza na waandishi wa habari, kwa niaba ya wenzake, kijijini hapo, Januari 20, 2026, Mbukwa amesema pamoja na kukamatwa kwake, mabalozi watatu wa kijiji hicho wanaendelea kusakwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika katika uharibifu wa mazingira, ikiwemo madai ya kuwaruhusu wageni kutoka Malawi kujihusisha na biashara haramu ya uchomaji mkaa.
Hata hivyo, mwenyekiti huyo amekanusha vikali madai ya kuwapokea wageni kutoka nchi jirani ya Malawi, akisisitiza kuwa raia huyo aliishi katika kijiji hicho muda mrefu kabla hata hajachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji.
Amesema hadi sasa uamuzi uliopo ni pamoja na kutojihusisha na usimamizi wa shughuli zozote za maendeleo mpaka pale utakapopatikana mwafaka wa kujua chanzo cha kukamatwa na uongozi wa kata.
“Kutokana na uongozi wa kata kutothamini uongozi wa kijiji, tumejiondoa na hatupo tayari kushiriki katika kusimamia shughuli za maendeleo katika kijiji chetu,” amesema Mbukwa.
Kwa upande wake, Kefasi Mbisa, mjumbe wa serikali ya kijiji hicho, amesema wameungana na mwenyekiti wao kujiuzuru kutokana na uongozi wa kata kumkamata kiongozi wao bila sababu za msingi, huku akifanya msako kumkamata mmoja wa wananchi katika kijiji hicho bila viongozi wa kijiji kuwa na taarifa.
“Changamoto hii itaathiri usimamizi wa shughuli za maendeleo, kwani wananchi pamoja na wajumbe waliojiuzuru ndio nguzo ya kuhamasisha maendeleo, hivyo naomba viongozi wa wilaya kusuluhisha mgogoro uliopo baina ya viongozi wa kijiji na kata,” amesema Mbisa.
Mjumbe mwingine, Oscar Chisunga amesema kujiuzuru kwao kumetokana na uongozi wa kata kujifanyia uamuzi wa kwenda kijijini kwao kukamata wananchi.
“Kama viongozi wa kata wameona uongozi wa kata una changamoto ya kutosimamia mazingira wangekaa meza moja ikiwa ni pamoja na kuitisha mkutano wa hadhara kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira, lakini kukamata kiholela haikubaliki,” amesema Chisunga.
Alipotafutwa kuzungumzia malalamiko dhidi yake, Mtendaji wa Kata ya Hezya, Ibrahim Tusamare alikiri kutoa amri ya kukamatwa kwa mwenyekiti wa kijiji hicho pamoja na raia wa Malawi, akieleza kuwa wanahusishwa na vitendo vya uharibifu wa mazingira katika Hifadhi ya Msitu wa Namwanga, unaozungukwa na vijiji vinne.
Hata hivyo, Tusamare amesema bado hajathibitishiwa rasmi taarifa za kujiuzulu kwa viongozi wote wa Serikali ya kijiji hicho.
“Taarifa za kujiuzulu bado sijazipokea rasmi. Nikifika ofisini na kupata muhtasari wa kikao kilichofanya uamuzi huo, nitaeleza kwa upana,” ameeleza Tusamare.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Augustino Senga amesema mwenyekiti huyo pamoja na mwananchi mmoja walikamatwa kwa tuhuma za kujihusisha na uharibifu wa mazingira, lakini baadaye waliachiwa kwa dhamana huku uchunguzi ukiendelea.