Wadau waitwa kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalumu Kabanga  

Kasulu. Wanafunzi wenye mahitaji maalumu wa Shule ya Msingi Kabanga Mazoezi iliyopo Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kuwasaidia mahitaji muhimu ili wasome kwenye mazingira rafiki na hatimaye kufikia ndoto zao.

Wakizungumza leo Januari 21, 2026, mara baada ya kupokea mahitaji mbalimbali kutoka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kigoma ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mpango wa uwajibikaji wa kijamii wa taasisi.

 Wanafunzi hao wamesema  pamoja na kuendelea kupokea mahitaji muhimu lakini bado uhitaji ni mkubwa shuleni hapo.

Mwanafunzi, Timotheo Mapengu amesema kutokupata mahitaji muhimu shuleni hapo kumewafanya kushindwa kuzingatia masomo kwa umakini na wakati mwingine kutofanya vizuri kwenye masomo yao, hivyo endapo watapata mahitaji wataweza kufanya vizuri kitaaluma.

 “Pamoja na kuendelea kupokea mahitaji kutoka sehemu mbalimbali lakini bado hayakidhi, hivyo bado tunahitaji sare za shule madaftari na vitu vingine ikiwemo chakula, tunaomba wadau na Serikali kutochoka kutusaidia sisi wanafunzi wenye mahitaji maalumu,” amesema Mapengu.

Mwanafunzi mwingine, Ester Paulo amesema pamoja na kuwa wao ni wanafunzi wenye mahitaji maalumu katika shule hiyo lakini ni wanapata changamoto ya ukosefu wa taulo za kike, hali inayowafanya kukaa kwa kutokujiamini hasa wakiwa katika siku zao.

Baadhi ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu wa shule ya msingi Kabanga Mazoezi, iliyopo wilayani Kasulu, mkoani Kigoma.



Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Kulwa Goodluck amesema licha ya Serikali na wadau kusaidia vitu mbalimbali mara kadhaa, bado wanafunzi kulingana na mazingira yao ya ulemavu wanakuwa na uhitaji hivyo ni muhimu kwa wadau kuendelea kutoa misaada shuleni hapo.

“Kuna watoto wenye ulemavu wa akili ambao wanakuja shule na kurudi nyumbani, tuna watoto wenye ulemavu wa viungo wao wanalala hapa shuleni, tuna watoto wenye ualubino,  ambao hawasikii nao wanalala hapa shuleni, jumla tuna watoto 140,”amesema mwalimu Goodluck.

Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TRA Mkoa wa Kigoma, Kwizera Ntibakazi  amesema wana wajibu wa kurudisha sehemu ndogo ya kile wanachokipata kwa jamii na kuwanunulia mahitaji  muhimu ambayo thamani yake ni  Sh8 milioni.