Dar es Salaam. Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Koplo Erick Ndagwa (32) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na shtaka moja la kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi zenye uzito wa kilo 193.66.
Ndagwa ambaye ni mkazi wa Kihonda mkoani Morogoro na wenzake wawili ambao sio askari, wamefikishwa Mahakamani hapo leo Alhamisi, Januari 22, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 1375 ya mwaka 2026.
Mbali na Ndagwa, wengine ni Paul Blas, mkazi wa Mbezi Malamba Mawili na Tido Mkude (35) mkazi wa Mwakasege Kinyerezi.
Washtakiwa hao wamesomewa shtaka lao na wakili wa Serikali, Monica Matwe, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.
Wakili Matwe amedai, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa Desemba 6, 2025 katika Mtaa wa Masoka Kinyerezi wilaya ya Ilala, walikutwa wanasafirisha bangi zenye uzito wa kilo 193.66.
Washtakiwa baada ya kusomewa shtaka lao, hakimu Makube aliwaeleza hawakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Pia kiasi cha dawa walichokamatwa nacho haina dhamana.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi haujakamilika, hivyo wanaomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa kutajwa.
Hakimu Makube aliahirisha kesi hadi Februari 4, 2026 kwa kutajwa na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na sababu alizozieleza Hakimu.