Tanga. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka watu wanaojihusisha na biashara ya kubadilisha fedha za kigeni kuacha moja kufanya shughuli hiyo kinyume cha sheria na kufuata taratibu zilizowekwa ili waweze kupatiwa leseni rasmi za kufanya biashara hiyo.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia uwepo wa baadhi ya watu wanaofanya biashara hiyo kiholela katika maeneo mbalimbali mkoani humo, hali inayokiuka sheria za fedha za nchi.
Akizungumza kwenye banda la Benki Kuu ya Tanzania wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Fedha Kitaifa yanayofanyika katika viwanja vya Usagara jijini Tanga, Ofisa Mwandamizi Mkuu kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha BoT, Mwile Kauzeni amesema biashara hiyo inapofanywa nje ya mfumo rasmi inaleta madhara makubwa kiuchumi.
Kauzeni amesema kuwa endapo biashara hiyo itaendelea kufanywa kinyume cha sheria, nchi itashindwa kubaini kiasi cha fedha kinachoingia na kutoka nchini, jambo linaloathiri udhibiti wa uchumi wa taifa.
Amesisitiza kuwa wanaofanya vitendo hivyo wanakiuka sheria na wanapaswa kuchukuliwa hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.
Akizungumzia utapeli wa kifedha unaofanywa mitandaoni, Kauzeni amewatahadharisha wananchi kutojihusisha kibiashara na watoa huduma za fedha ambao hawajatambuliwa na Benki Kuu ya Tanzania, akisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda fedha za wananchi dhidi ya watu wenye nia ovu.
“Niwatake wananchi wafahamu kuwa BoT ina orodha ya watoa huduma za fedha mtandaoni waliopata leseni rasmi. Hadi sasa tuna wakopeshaji wa kidijitali 18 waliothibitishwa, na wananchi wanashauriwa kutembelea tovuti rasmi ya BoT ili kupata taarifa sahihi kabla ya kuanza kushiriki kwenye biashara hizo,” amesema Kauzeni.
Mchambuzi wa masuala ya kifedha kutoka Kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za Fedha BoT, Charles Kanuda akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.
Ameongeza kuwa BoT inashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kudhibiti majukwaa ya kifedha yasiyo halali, ambapo majukwaa yanayobainika kufanya shughuli bila kibali hufungiwa, hatua ambayo imefanikiwa kupunguza kwa kiasi kikubwa malalamiko kutoka kwa wananchi.
Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya fedha kutoka kurugenzi ya Ustawi na Huduma Jumuishi za fedha Benki Kuu ya Tanzania, Charles Kanuda, amesema serikali imeanzisha Mfuko wa Uthamini wa Mikopo unaolenga kusaidia Watanzania wanaohitaji mikopo lakini hawana dhamana ya kutosha.
Kanuda amesema kupitia mfuko huo, mkopaji anaweza kupata dhamana ya hadi asilimia 75 ya mkopo anaouhitaji mradi benki iwe tayari kutoa mkopo huo, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa mitaji na kuchochea ukuaji wa biashara.
Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkwakwani, Mwajuma Kileo, amesema baada ya kutembelea banda la Benki Kuu wamejifunza mbinu za kutambua fedha bandia kwa kutumia alama za usalama, maarifa ambayo hata wanafunzi aliokuwa nao walifurahia na kunufaika nayo.
Naye Adrus Mahmood, mwanafunzi wa shule hiyo, amesema ziara hiyo imemsaidia kuongeza uelewa wake wa kutofautisha noti halali na bandia, tofauti na awali ambapo alikuwa hana uelewa wa kutosha.
Hatua zinazochukuliwa na Benki Kuu ya Tanzania zinaonesha dhamira ya serikali katika kulinda uchumi wa nchi na usalama wa fedha za wananchi.
Kupitia elimu, udhibiti na ushirikiano na taasisi nyingine, BoT inaendelea kuhimiza matumizi ya mifumo rasmi ya kifedha ili kujenga uchumi imara, salama na jumuishi kwa maendeleo endelevu ya taifa.