Mwanza. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando, iliyopo jijini Mwanza imeanza kutoa huduma ya upasuaji wa kisasa wa matundu madogo kwa wagonjwa wenye matatizo ya magoti na vifundo vya miguu.
Hatua hiyo inalenga kupunguza gharama na mateso kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa na maeneo ya jirani.
Awali, wagonjwa waliokuwa wakifika Bugando walihudumiwa kwa kupewa dawa za kupunguza maumivu au kufanyiwa upasuaji wa kupasua magoti na vifundo, lakini sasa huduma hiyo imeboreshwa na kuwa ya kisasa zaidi.
Huduma hiyo mpya inaleta ahueni pia kwa wanamichezo, hususan wachezaji wa soka, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikumbwa na majeraha ya vifundo vya miguu. Bugando imekuwa hospitali ya kwanza katika ukanda huo kuanza kutoa upasuaji wa kisasa wa kifundo cha mguu kwa kutumia njia ya matundu madogo.
Hospitali hiyo imeanzisha huduma ya Arthroscopy kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Shirika la Hope Ministry la Marekani kupitia kambi maalumu ya matibabu.
Tangu Januari 19, 2026, jumla ya wagonjwa 12 kati ya 65 waliogundulika kuwa na uhitaji wa huduma hiyo wamefanyiwa upasuaji.
Akizungumza leo Alhamisi Januari 22, 2026 hospitalini hapo, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji Bugando, Dk Samson Kichiba amesema kuanza kwa huduma hiyo ni hatua muhimu katika kupunguza mateso kwa wananchi wa Kanda ya Ziwa, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakihangaika na maumivu ya magoti na vifundo vya miguu.
Amesema matatizo ya magoti na vifundo vya miguu ni changamoto kubwa za kiafya zinazowaathiri watu wa rika na fani mbalimbali, wakiwemo wanamichezo na watu wanaofanya kazi nzito.
“Upasuaji wa matundu madogo una faida nyingi, ikiwemo kidonda kuwa kidogo, kuharakisha mchakato wa kupona kwa wagonjwa, kupunguza muda wa kulazwa hospitalini na kupunguza hatari zinazohusiana na upasuaji wa kawaida,” amesema Dk Kichiba.
Amesema huduma hiyo mpya inatarajiwa kupanua wigo wa matibabu katika Hospitali ya Bugando na kusaidia jamii kwa ujumla, huku ikichangia kuimarisha afya za Watanzania.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Mifupa Bugando, Danny Matari amesema awali hospitali hiyo ilikuwa ikipokea kati ya wagonjwa 40 hadi 50 kwa siku wenye matatizo ya magoti na vifundo vya miguu, lakini wengi wao walilazimika kupewa rufaa kwenda Muhimbili au nje ya nchi kutokana na kukosekana kwa huduma hiyo Bugando.
Amesema baada ya kuanza kwa huduma hiyo, hakutakuwa na ulazima wa kumsafirisha mgonjwa yeyote nje ya Bugando kwa sababu hospitali sasa ina wataalamu na vifaa tiba vya kisasa, baada ya kuwezeshwa na Shirika la Hope Ministry la Marekani, ambalo pia limetoa mafunzo kwa madaktari wa hospitali hiyo.
Timu ya wataalam kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando wakifanya upasuaji wa magoti na vifundo vya miguu, kwa njia ya matundu madogo ambayo imeanzishwa rasmi hospitalini hapo na kuleta nafuu kwa wagonjwa waliokuwa wakilazimika kupewa rufaa.
“Huduma hii imewafuata wananchi walipo. Wakazi wa Kanda ya Ziwa na maeneo ya jirani sasa watanufaika kwa kiasi kikubwa kwa kupata huduma hii karibu na makazi yao,” amesema.
Naye mwakilishi wa Shirika la Hope Ministry, Dk Gayle Stroschein, amesema lengo la ushirikiano huo ulioanza mwaka 2024 ni kuhakikisha huduma hiyo inakuwa endelevu kwa kuwajengea uwezo madaktari wa ndani.
“Tumejikita kuwafundisha madaktari wa Bugando namna ya kufanya upasuaji wa Arthroscopy ili huduma hii iendelee kutolewa hata baada ya sisi kuondoka,” amesema.