Dar es Salaam. Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe amesema jamii inakabiliwa na utapiamlo unaotokana na lishe duni unaochangiwa na kukosekana kwa elimu ya kupika vyakula vilivyopo.
Amesema kutokana na hali hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan aliingia mikataba ya lishe na wakuu wa mikoa, wilaya na viongozi mbalimbali kwa lengo kuimarisha utoaji wa elimu ya namna ya ulaji bora kwa wananchi.
Dk Shekalaghe ametoa kauli hiyo leo Alhamisi, Januari 22, 2026 jijini Dodoma katika mkutano wa tathmini ya mkataba wa lishe kwa mwaka 2024/2025.
“Jamii inakabiliwa na utapiamlo unaotokana na lishe duni inayochangiwa na kukosekana kwa elimu ya kupika vyakula vilivyopo hali iliyomfanya Rais Samia kuingia mikataba ya lishe na wakuu wa mikoa,” amesema.
Dk Shekalaghe amesema katika utekelezaji wa mikataba hiyo ya lishe wamefanya mapitio ya sera ya afya ya 2007 kujumuisha na masuala ya lishe kuendana na hali halisi.
“Tumeongeza wataalamu wa lishe ambapo hivi sasa Serikali inatoa ufadhili wa masomo ya lishe kwa ngazi ya stashahada, mtaala ambao wizara ya afya tumeanzisha,” amesema.
Juhudi nyingine wanayofanya ni kufanya mapitio ya urutubishaji wa vyakula hususan mchele.
Amefafanua ni lazima kuwe na kanuni na taratibu za urutubishaji wa vyakula ili kumlinda mlaji.
“Pia tumesimamia matibabu ya utapiamlo mkali, tumetenga uniti kwa watoto wanaopata utapiamlo mkali wapate huduma na kurejea katika hali ya kawaida,” amesema.
Juhudi zingine za kuimarisha afya anazotaja mtaalamu huyo ni utoaji wa matone ya vitamin A na dawa za minyoo kwa watoto pamoja na kuanzisha mradi wa watoa huduma wa afya ngazi ya jamii.
Dk Shekalaghe amesema kazi yao kubwa ni kutoa elimu ya lishe kwa jamii.
Amesema kunapokuwa na lishe bora kunachagiza tija katika shughuli zote za kiuchumi anazofanya binadamu.
“Bila lishe bora hatuna jamii yenye afya, usipokuwa na jamii yenye afya maana yake hatuna nguvu kazi ya kufanya kazi ya kusaidia kukuza uchumi,”amesema.
Kutokana na kukosekana kwa nguvu kazi hiyo, Dk Shekalaghe amesema hakutakuwa na uchumi ulioimarika.
Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayesimamia ustawi wa jamii na lishe, Profesa Tumaini Nagu amesema Ofisi ya Waziri Mkuu Tamiseni ina jukumu la kuratibu shughuli zote zinazofanyika mikoani na halmashauri ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Tunaendelea kusimamia utoaji wa huduma za lishe katika mikoa na halmashauri zetu zote, niwashukuru wakuu wa mikoa wote kwa kusimamia mikataba ya lishe katika maeneo yao,” amesema.
Profesa Nagu amesema katika utekelezaji wa mikataba hiyo wakuu wa mikoa, makatibu tawala na wakuu wa wilaya pamoja na watendaji ndani na nje ya sekta ya afya wameshirikiana kuitekeleza.