SINGIDA Black Stars kama ilivyo kawaida, dirisha hili kikosi chake kimepanguliwa tena baada ya kuondoka kwa baadhi ya wachezaji nyota.
Tunasema ni kawaida kwa sababu karibia kila dirisha la usajili liwe kubwa au dogo, timu hiyo kutokea katikati ya Tanzania imekuwa ikiondokewa na wachezaji muhimu kikosini na wengi wao huenda timu za hapahapa Bongo.
Kwa kuhesabu tu katika dirisha hili, Clatous Chama na Clement Kibabage wamejiunga na Simba, Mohamed Damaro yupo zake Yanga hivi sasa na kuna Idriss Diomande ambaye yuko mbioni kutua Azam FC.
Hapo bado kuna taarifa za mchezaji Andrew Phiri nafasi ya ushambuliaji ambaye inaripotiwa ameenda Ureno kufanya majaribio katika klabu mojawapo ya huko ili kuona kama anaweza kujiunga nayo na kuachana na Singida BS.
Dirisha kubwa la usajili kabla ya msimu kuanza, timu hiyo iliondokewa na Frank Assinki, Jonathan Sowah, Ibrahim Imoro, Arthur Bada na Edmund John ambao wengi walibaki hapa na mmoja alienda nje ya nchi ambako yupo hadi leo.
Pamoja na muendelezo wa wachezaji wake muhimu kuondoka katika kila dirisha, Singida Black Stars imeonekana kuwa madhubuti katika kuziba mapengo ya hao wanaoondoka kwa kusajili nyota ambao wamekuwa na ubora wa hali ya juu kiasi cha kuvutia timu nyingine.
Sajili zao mara nyingi zimekuwa zikiziba vyema mapengo ya wale ambao wameondoka na timu haionekani kutetereka sana kulinganisha na baadhi ya klabu ambazo zimekuwa zikihaha kuziba nafasi za nyota wao pindi wanapotimka.
Singida BS ni timu ambayo inaonekana imejipanga vyema katika ufanyaji skauti wa wachezaji kabla ya kuwasajili na ndiyo maana huwa haigopi kuachia wachezaji wake muhimu kuondoka katika madirisha ya usajili.
Wanajua wao wana utaalamu wa kuvua samaki huku klabu nyingine zikihitaji zaidi samaki hivyo hata wakiwapa, bado kesho na keshokutwa watawafuata tena.