MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, Hamis Kiiza ‘Diego’ amemtabiria makubwa kiungo mpya wa timu hiyo, Allan Okello ‘Star boy’, huku akisema Yanga imelamba dume kwa nyota huyo wa Uganda akiamini atafanya mambo makubwa ndani ya klabu hiyo na kuandika rekodi yake mwenyewe huku akiitaja nidhamu yake kuwa ndio itakayombeba.
Wakati huo huo amebariki Star Boy kuvaa jezi namba 20 aliyopewa katika kikosi cha Yanga akimhakikishia ni namba sahihi na ni ya bahati hivyo anaamini ataitendea haki.
Okello ni usajili mpya wa Yanga katika dirisha dogo akijiunga akitokea Vipers ya Uganda na tayari ameanza kuitumikia timu hiyo kwenye mechi ya Ligi Kuu akiwa sehemu ya kikosi hicho kilichoshinda mabao 6-0 dhidi ya Mashujaa FC.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kiiza aliyewahi pia kutamba na Simba na Kagera Sugar alisema nyota huyo ametua katika timu sahihi na anamuona akifanya mambo makubwa ndabi ya timu hiyo kutokana na kipaji alichonacho lakini pia nidhamu.
“Star Boy ni kipaji kikubwa na nichezaji mwenye nidhamu kubwa ndani na nje ya uwanja akipewa ushirikiano mzuri kuanzia uongozi, benchi la ufundi na wachezaji kwa jumla namwamini na anajitambua atafanya mambo makubwa,”
“Ni kweli kuna rekodi tamu na nzuri zimeandikwa na wachezaji wa kutoka Uganda waliopita Yanga nikiwemo mimi, naamini pia ana nafasi nzuri ya kufanya makubwa na kuandika rekodi yake mwenyewe.”
Akizungumzia jezi namba 20 aliyokuwa akiivaa akiwa Yanga Kiiza alisema ni namba ya bahati hajakosea kuivaa anaamini ataitendea haki kwa kufanya mambo makubwa ndani ya Yanga.
“Okello yupo sehemu sahihi namtakia kila lakheri namuamini najua hawezi niangusha atafanya vitu vingi bora na kuisaidia Yanga kufikia mafanikio katika malengo yao ndani na nje.”
Jezi namba 20 ukiondoa Kiiza Yanga imevaliwa na Zawadi Mauya na Jonas Mkude baada ya kujiunga na timu hiyo akitokea Simba.