Kocha Simba aagiza beki kutoka Yanga

YANGA ikiwa inapiga hesabu za kufunga dirisha la usajili baada ya awali kutambulisha mashine nne mpya, kuna jipya limeibuka kutokea Morocco baada ya kocha wa zamani wa Simba, Fadlu Davids amedaiwa kutaka kuchomoa beki mmoja wa klabu hiyo.

Iko hivi. Kocha Fadlu anayekinoa kwa sasa kikosi cha Raja Casablanca ya Morocco, amewaambia mabosi wa klabu hiyo anamtaka beki wa kushoto na chaguo lake la kwanza ni Chadrack Boka aliyepo Yanga.

Baada ya ombi hilo la Fadlu kufika kwa mabosi wa klabu hiyo, taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti maafisa wa Raja fasta wamepiga hodi Yanga kuangalia uwezekano wa kufanikisha dili hilo.

KOCH 01


“Maafisa wa Raja ambayo inafundishwa na Fadlu wamepiga hodi Yanga wakitaka huduma ya Boka kama watakuwa tayari kumuachia na mchezaji mwenyewe utayari wake wa kwenda kuanza maisha mapya Morocco,” kilisema chanzo kutoka Yanga na kuongeza;

“Hata hivyo, Raja inafahamu dili hilo halitakuwa rahisi, kwani Boka bado anahitajika Yanga akicheza beki wa kushoto akipishana na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.”

KOCH 02


Mwanaspoti lilimpata mmoja wa viongozi wa Yanga na alikiri, Raja imeonyesha nia ya kumtaka Boka, hata hivyo haitakuwa rahisi kuamwachia kutokana na hesabu zao zilivyo kwa sasa.

“Boka anatakiwa na Raja, naona Fadlu anataka kumsajili lakini bado yuko katika hesabu zetu, wachezaji tuliowafungulia milango walishaondoka. Kule kushoto hesabu tulishazifunga, kuna Boka na Tshabalala, ukiangalia hapa nchini hawa ndio mabeki wenye uwezo mkubwa, sioni nafasi ya hiyo biashara kufanyika labda ofa ije kubwa zaidi, tumewaambia walete ofa yao tuiangalie,” alifichua bosi huyo.

KOCH 04


KOCH 04

Kama Yanga itaendelea kuweka ugumu kumuachia Boka, maana yake Raja inaweza kumtumia beki huyo kununua mkataba endapo anataka kuachana na mabingwa hao wa soka Tanzania.

Boka alisajiliwa msimu uliopita kuziba nafasi ya Joyce Lomalisa aliyerejea Angola na amekuwa na kiwango bora na kuwa katika kikosi cha kwanza kabla ya ujio wa Tshabalala msimu huu uliomfanya awe anapokezana naye katika kikisi hicho cha kwanza kulingana na mechi husika.

KOCH 03


Ili kununua mkataba wa Boka hali itakayofanya kuondoka Yanga kirahisi, kiasi cha Dola 350,000 (Sh878.9 milioni za Tanzania) kinapaswa kutolewa kwani ndiyo masharti yaliyopo wakati anasaini mkataba wa kutua hapo mwanzoni mwa msimu wa 2024-2025 akitokea FC Lupopo ya kwao DR Congo.

Boka amebakiza miezi sita pekee kwenye mkataba wake na Yanga na mwisho wa msimu huu atakuwa mchezaji huru na anaweza kuondoka bure endapo dili hilo litakwama sasa na ikitokea hatoongeza muda mwingine wa kuichezea timu hiyo.