Geita. Jeshi la Polisi mkoani Geita limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya baadhi ya wachimbaji wadogo waliokuwa wameandamana, wakidai mmiliki wa leseni ya uchimbaji kupunguza malipo ya ubia katika shughuli za uchimbaji wa dhahabu.
Baadhi ya wachimbaji hao, wamedai kuwepo kwa ukosefu wa usawa katika mgao wa mifuko ya mawe yenye dhahabu, wakieleza kuwa hali hiyo imesababishwa na madai ya kuongezeka kwa ushuru wa Serikali unaotaka mwekezaji na Serikali kupata mgao sawa wa asilimia 50, hali iliyowaacha wachimbaji wadogo bila mgawanyo ulio wazi.
Wakizungumza leo Alhamisi Januari 22, 2026, wachimbaji hao wamesema awali walikuwa wakilipwa mifuko miwili ya mawe katika kila mifuko 10, baada ya kutoka kwenye duara la uchimbaji.
Lakini wanasema hali ni tofauti na sasa baada ya kuwepo kwa tetesi za kupanda kwa tozo hizo, wanalipwa nusu ya mfuko au posho ndogo inayokadiriwa kulingana na siku husika.
Mchimbaji katika Mgodi wa Msasa, Saimon Mathias alizungumza na Mwananchi amelalamikia kile alichokitaja kuwa kukosekana kwa usawa kati ya wachimbaji wadogo na mmiliki wa mgodi, akieleza kuwa wachimbaji ambao ndio watendaji wa kazi wanapitia hali ngumu ya kiuchumi.
“Hapo mwanzo mtendaji alikuwa anapata mifuko miwili kati ya kumi, lakini sasa mwenye duara anachukua asilimia 50 na mwenye leseni asilimia 50. Mtendaji anabaki na nusu ya mfuko, wakati yeye ndiye anayeshuka chini kufanya kazi ngumu,” amesema Mathias.
Wachimbaji wadogo mgodi wa Msasa wilayani Bukombe.
Naye Kiura Daniel, mchimbaji mdogo katika eneo hilo amesema kwa sasa hakuna utaratibu ulio wazi wa malipo kwa wachimbaji wadogo, hali iliyosababisha kusimama kwa shughuli za uchimbaji.
“Uchimbaji hauendelei mpaka sasa. Wamesema Serikali inataka mgao wa hamsini kwa hamsini kati ya mwenye eneo na Serikali, lakini wachimbaji hawana pa kujitetea. Unaweza kufanya zamu ya usiku, ukitoka asubuhi unakadiriwa kulipwa Sh5,000 au Sh10,000 tu,” amedai Kiura.
Leo asubuhi kupitia mitandao ya kijamii, zilisambaa taarifa zikidai kuwa baadhi ya watu wamejeruhiwa na baadhi kuuawa baada ya polisi kudaiwa kutumia risasi za moto kuwatawanya waandamanaji.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bukombe, Paskasi Mragili amekanusha madai hayo.
Akizungumza kwa simu na Mwananchi, Mragili amesema polisi wametumia mabomu ya machozi baada ya kubaini kuwa baadhi ya watu walikuwa na nia ya kuiba mifuko ya mchanga wenye dhahabu iliyokuwa mali ya mwekezaji katika eneo hilo.
Amesema kutokana na mvua kubwa iliyonyesha jana, wasimamizi wa usalama mgodini kwa kushirikiana na mmiliki wa leseni waliamua kusitisha shughuli za uchimbaji kwa muda, kwa kuwa eneo hilo lipo kwenye majaruba yenye maji mengi, hali iliyohatarisha usalama wa wachimbaji, lakini uamuzi huo ulitafsiriwa tofauti na baadhi ya wachimbaji.
“Eneo limezungushiwa mabati na ndani kuna mifuko yenye mawe ya thamani. Baadhi ya watu walitaka kutumia fursa hiyo kufanya hujuma na kuiba mifuko hiyo, hivyo kundi likajikusanya na kutaka kuingia kwa nguvu,” amedai Mragili.
Ameongeza kuwa baada ya hali hiyo kuzidi, uongozi wa mgodi uliomba msaada wa Jeshi la Polisi ili kutuliza hali, hatua iliyosababisha matumizi ya mabomu ya machozi na kwa sasa eneo hilo limetulia isipokuwa watu wachache wanaodaiwa kuendelea kuhamasisha kurejea kwa nia ya wizi.
Mragili amekanusha taarifa za vifo inayosambazwa mitandaoni, akisema watu wawili pekee wamepata majeraha madogo. Amesema mmoja ni mwananchi aliyekatwa sikio na bati alipokuwa akikimbia wakati wa vurugu, na mwingine ni askari polisi aliyejeruhiwa baada ya kuanguka na kugonga kitu chenye ncha kali, na kwa sasa wote wameshatibiwa.
“Hatuna mtu aliyefariki wala askari aliyekatwa na mapanga kama inavyodaiwa. Wote waliopata majeraha wametibiwa na hali zao ni nzuri,” amesema.
Kufuatia kusitishwa kwa shughuli za uchimbaji, Serikali imeagiza wataalamu wa madini kufika katika eneo hilo ili kujiridhisha na hali ya kiusalama, baada ya maji kupungua, kabla ya kutoa tamko rasmi la kuendelea na shughuli za uchimbaji.
Kwa upande wake, mmiliki wa leseni ya mgodi huo, Cosmas Ignas amekanusha madai ya kuongezwa kwa tozo ya asilimia 50, akisema kusitishwa kwa uchimbaji kulitokana na kujaa kwa maji baada ya mvua kubwa, huku akidai kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa eneo hilo.
“Vurugu hizi zimetokea baada ya mvua kubwa kunyesha. Tulisitisha uzalishaji kwa sababu za usalama kama tunavyofanya mara kwa mara. Baadhi ya watu walikuwa na nia ya wizi, si madai ya asilimia 50 kama wanavyosema,” amesema Ignas.