Masilahi bora ya wafanyakazi yatajwa msingi wa ufanisi Tanesco

Dodoma. Masuala ya masilahi na haki za wafanyakazi yanatajwa kupewa kipaumbele  katika juhudi za kuimarisha ufanisi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), huku Serikali ikisisitiza usimamizi madhubuti na ushirikiano kazini kama nguzo muhimu za utoaji wa huduma bora za umeme nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Januari 22, 2026 na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi wakati akifungua rasmi kikao cha 55 cha Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Tanesco kinachofanyika mkoani Dodoma.

Akizungumza katika ufunguzi wa kikao hicho, Waziri Ndejembi ameishukuru Serikali kwa kuboresha masilahi na stahiki za wafanyakazi, hatua aliyoeleza kuwa imeongeza morali na ufanisi kazini.

Amesisitiza umuhimu wa kusimamia haki za wafanyakazi, kuimarisha ushirikiano mahali pa kazi na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu masuala yanayohusu huduma ya umeme.

“Natambua mmekutana hapa kujadili kwa kina mambo yanayowahusu wafanyakazi; naomba mhakikishe mnazungumza yote kwa uwazi na kufikia makubaliano yatakayosaidia kuboresha utendaji wa shirika na masilahi ya wafanyakazi,” amesema Waziri Ndejembi.

Aidha, amewahimiza viongozi na wafanyakazi wa shirika hilo la umeme nchini, kuendelea kuboresha utoaji wa huduma bora za uhakika na endelevu za umeme kwa wateja wote nchini.

Awali, akimkaribisha Waziri Ndejembi katika kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Lazaro Twange, alimshukuru kwa kukubali kufungua kikao hicho na akamuhakikishia kuwa uongozi wa shirika utaendelea kusimamia haki za wafanyakazi na kuhakikisha mijadala ya kikao hicho inaleta matokeo chanya katika utendaji.