Dodoma. Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, ametoa maagizo matano kwa Maofisa Madini wa Mikoa (RMOs), akiwataka kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika utekelezaji wa majukumu yao na kuepuka kuwa chanzo cha migogoro kwenye maeneo ya uchimbaji madini.
Aidha, amewaonya wamiliki wa leseni za utafiti wa madini ambazo hazijafanyiwa kazi kujiandaa kufutiwa, akisema Serikali itafanya ukaguzi maalumu wa kampuni zinazomiliki leseni nyingi bila kuzifanyia kazi.
Akizungumza leo Alhamisi, Januari 22, 2026 jijini Dodoma wakati wa kikao cha Menejimenti ya Tume ya Madini, Mavunde amesema mafanikio yanayoonekana, yakiwemo ongezeko la ukusanyaji wa mapato na uboreshaji wa miundombinu ya utendaji kazi kama ujenzi wa jengo la kisasa la Tume ya Madini, ni matokeo ya usimamizi thabiti wa rasilimali za nchi kwa manufaa ya Watanzania.
Ameipongeza Tume ya Madini kwa usimamizi mzuri na kuwataka RMOs kuongeza bidii, uwajibikaji na ushirikiano ili kuleta maendeleo zaidi katika sekta hiyo.
Waziri huyo amesisitiza umuhimu wa RMOs kufanya kazi kwa mshikamano na kuondoa tabia ya kufanya kazi kama ofisi zinazojitegemea, akibainisha kuwa changamoto nyingi zinaweza kutatuliwa kwa ushirikiano.
Pia ameelekeza kuimarishwa kwa uadilifu na maadili kazini, akiwataka RMOs kusimamia nidhamu ya watumishi walio chini yao, huku akionya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya atakayeshindwa kusimamia ipasavyo.
“Endapo nitalazimika mwenyewe kushuka kwenda kutatua mgogoro katika mkoa wowote, RMO husika ajihesabu kuwa siku zake zinahesabika. Baadhi ya migogoro inasababishwa na matumizi mabaya ya mamlaka ya utoaji leseni, hususan kwa wachimbaji wadogo,” amesema.
Mavunde amewataka RMOs kuwasilisha ndani ya siku saba orodha ya leseni kubwa na leseni za utafiti zisizofanyiwa kazi katika mikoa yao, akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia tabia ya watu kuchukua maeneo ya madini kwa lengo la kusubiri wawekezaji.
Ameongeza kuwa Serikali itafanya ukaguzi maalumu wa kampuni zinazomiliki leseni nyingi, akibainisha kuwa taarifa za uongo kuhusu umiliki au matumizi ya leseni ni kosa kisheria.
Pia ameelekeza utekelezaji wa mfumo wa kielektroniki wa utoaji leseni (e-Leseni), akimtaka Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kuhakikisha unaanza kutumika rasmi ifikapo Juni 30 mwaka huu.
Amesema mfumo huo utapunguza mwingiliano wa ana kwa ana, kuongeza uwazi, kupunguza malalamiko na kuwalinda maofisa dhidi ya tuhuma zisizo za msingi.
Amesisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa Sheria, Kanuni na Taratibu za madini ni msingi wa utulivu, haki na maendeleo endelevu ya sekta hiyo.
Mavunde amesema mchango wa sekta ya madini katika Mfuko Mkuu wa Serikali unaendelea kuongezeka, ambapo kwa mwaka huu wa fedha Serikali imeweka lengo la kukusanya shilingi trilioni 1.2, akieleza kuwa lengo hilo linawezekana kufikiwa.
“Ifikapo Juni 30 tunataka kuona mfumo unasoma trilioni 1.2. Dalili zinaonyesha hilo linawezekana, hasa ikizingatiwa kuwa tayari mmekusanya zaidi ya Sh719 bilioni,” amesema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa, ameipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka malengo ya ukusanyaji mapato na kuwataka kuongeza kasi ili kufikia na kuvuka lengo la Sh1.2 trilioni.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Janeth Mwakashingo, amesema Tume inaishukuru Serikali kwa kuiwezesha kwa nyenzo mbalimbali ikiwemo magari kwa ajili ya RMOs, hatua iliyoongeza ufanisi wa utendaji kazi mikoani.
Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, tume ilikusanya Sh663.64 bilioni sawa na asilimia 108.99 ya lengo, ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 ikilinganishwa na makusanyo ya awali.