Dar es Salaam. Mchungaji Enock Likoma ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kisutu jinsi alivyoshawishiwa na kampuni ya Vanilla International Limited kwa kuwekeza pesa katika kampuni hiyo inayojishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali.
Mchungaji Likoma ameeleza hayo wakati akitoa ushahidi wake katika kesi ya uhujumu uchumi inayomkabili mkurugenzi mwanzilishi wa kampuni hiyo ya vanila, Simon Mkondya, maarufu Dk Manguruwe na mwenzake John Rwezaula.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na jumla ya mashitaka 28 yakiwemo ya kujipatia pesa zaidi ya Sh90 milioni kwa udanganyifu na utakatishaji fedha kwa kununua viwanja tisa eneo la Idunda Mkoa wa Njombe.
Katika ushahidi wake, akiongozwa na mwendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Edith Mauya amedai kuwa aliahidiwa na kampuni hiyo kuwa akiwekeza Sh3.2 milioni kwenye zao la maharage atapata faida ya Sh6.5 milioni ndani ya miezi sita tu.
Mchungaji Likoma ambaye amesema anafanyia shughuli zake Vingunguti bila kutaja kanisa lake, amedai kuwa aliifahamu kampuni hiyo kupitia vyombo vya habari mwaka 2022.
Amedai kuwa aliifahamu kampuni hiyo kwamba inajihusisha na kilimo cha mazao mbalimbali ikiwemo vanilla na maharage baada ya kumsikiliza mkurugenzi wake, Dk Manguruwe.
“Baada ya kusikia matangazo hayo, nilienda ofisi za kampuni hiyo eneo la Mwenge, mkabala na Mlimani City kupata maelekezo zaidi kuhusu kilimo hicho cha vanilla, niwekeze endapo nitaridhika, ” amesema Mchungaji Likoma na kuongeza:
“Nilikutana na dada Dina Mchalo ambaye alinipa maelekezo kuhusiana na uwekezaji na mimi niliwekeza katika kilimo cha maharage, nikipewa namba ya akaunti ya Vanilla International, nikaenda kuweka Sh3.2 milioni.”
Amesema walimuandikia mkataba wakisema baada ya miezi sita mkataba huo utakuwa umemalizika na katika uwekezaji huo aliambiwa baada ya miezi sita angepeta faida ya Sh6.5 milioni.
Baada ya miezi sita kuisha, alirudi ofisi za Vanilla ambako alikutana na mshtakiwa wa pili, John Rwezaula, ambaye alimwambia kilimo cha maharage hakikufanya vizuri kutokana na hali ya hewa, hivyo kampuni haikuzalisha kitu chochote.
Pia, Rwezaula alimwambia kuwa watampatia kitalu cha vanilla kama mbadala wa maharage na kwa mkataba wa mwaka mmoja na nusu ndio apate faida.
Vilevile Rwezaula alimwambia kwa kuwa pesa zake Sh6.5 milioni hazikupatikana basi watamhamishia katika kitalu cha vanilla cha mita za mraba 80 ambacho kitakuwa na thamani ya Sh36 milioni baada ya mwaka mmoja na nusu.
Alirudi nyumbani na baada ya muda aliwatafuta ili aende akaangalie shamba, lakini walimwambia shamba lipo Arusha na kuwa muda wa wawekezaji kwenda kuangalia shamba haujafika na ukifika watamjulisha.
“Mwisho wa siku simu zilikuwa hazipokelewi, nilirudi ofisini kwao nikakuta zimefungwa, baada ya muda nilisikia katika vyombo vya habari kwamba Mkurugenzi wa kampuni ya Vanilla International Limited Simon, amekamatwa, ” amesema na kuhitimisha:
“Baadaye niliona amefikishwa mahakamani, hivyo nilienda kituo cha Polisi Kati (Kituo Kikuu), kuandika maelezo kuhusiana na Simoni Mkondya.”
Awali, shahidi wa tano, Rebecca Msuya (52) mkazi wa Kibaha mkoani wa Pwani na mjasiriamali pia ameieleza Mahakama kuwa aliifahamu kampuni hiyo ya Vanilla kupitia vyombo vya habari, ambapo mkurugenzi mwenyewe, Mkondya ndio alikuwa anaielezea.
Amesema kuwa Mkondya alijieleza kampuni yake kuwa inajishughulisha na masuala ya kilimo cha mazao mbalimbali kama vanilla, soya na mengine.
Baada ya kusikia matangazo hayo, alichukua hatua ya kwenda ofisi kwao, katika jengo la City Mall, ambako alikutana na mmoja wa wafanyakazi asiyemkumbuka jina, aliyempa maelezo ya kina kuhusu kilimo cha zao la soya akavutiwa nayo.
Hivyo aliamua kuwekeza Sh1.2 milioni katika zao la soya kwa matarajio ya kutapata Sh2.5 milioni na akaambiwa kuwa shamba lake lipo eneo la Nduruma, Arusha na kwamba lina ukubwa wa nusu ekari.
“Baada ya maelekezo hayo, nilichukua hela na kwenda kulipa kwenye akaunti ya kampuni ya Vanilla katika Benki ya CRDB, Oktoba 27, 2022. Nililipa Sh1 milioni na nilienda na risiti ya benki ofisi za Vanilla wakaigonga muhuri wa ofisi, nikatulia kwa ajili ya kusubiri faida yangu,” amesema.
Hata hivyo, amesema kuwa Februari 2023 alipigiwa simu na mmoja wa wafanyakazi akamtaka aende ofisini.
Alipokwenda alikutana na mfanyakazi wa kike aitwaye Jovita ambaye alimwambia kuwa analima nusu heka hivyo anatakiwa atoe Sh1.2 milioni na si Sh1 milioni.
Ilimlazimu aongeze palepale Sh200,000 na akapewa risiti iliyogongwa muhuri.
Kisha aliambiwa kuwa baada ya miezi sita ataanza kuvuna hivyo aliendelea kusubiri.
“Niliendelea kusubiri na baadaye niliona kama ninadanganywa hapa …nikaona kama ni nachezewa mchezo wa utapeli hapa…hivyo niliamua kwenda polisi.
Kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki itaendelea tena kesho Ijumaa, Januari 23, 2026, kwa mashahidi wengine wa Jamhuri.