Unguja. Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imezindua mfumo wa kidijitali wa usajili wa diaspora wenye asili ya Zanzibar, hatua iliyolenga kukabiliana na changamoto zilizokuwepo katika mfumo wa awali wa usajili wa kutumia makaratasi.
Inaelezwa kwamba hilo linakwenda sambamba na kuongeza ufanisi wa kuwatambua na kuwaunganisha na fursa za maendeleo zilizopo visiwani humo.
Kupitia mfumo huo, Serikali inatarajia kupata takwimu sahihi zitakazowezesha kuwaunganisha wanadiaspora na fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta za vipaumbele ikiwemo utalii, uchumi wa buluu, kilimo, afya, elimu, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) pamoja na viwanda.
Hayo yamebainika wakati wa uzinduzi wa mfumo huo ulioandaliwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA).
Akizungumza katika hafla hiyo leo Alhamisi Januari 22, 2026, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu, Dk Saada Mkuya Salum amesema mfumo huo ni hatua ya kimkakati katika kupanga, kuratibu na kuongeza tija ya mchango wa wanadiaspora katika maendeleo ya Zanzibar.
Amesema kupitia mfumo huo, serikali pia itakuwa na takwimu sahihi zitakazowawezesha kuwaunganisha wanadiaspora na fursa za uwekezaji katika sekta za kipaumbele zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira, mapato na maendeleo jumuishi.
“Sekta hizi zinahitaji ushiriki wa wanadiaspora wenye uwezo wa kuwekeza nyumbani,” amesema waziri huyo.
Dk Saada amesema hatua hiyo inaonesha dhamira ya serikali ya kutumia teknolojia ya kidijitali kama nyenzo muhimu ya utekelezaji wa sera, utoaji wa huduma na usimamizi wa rasilimali watu kwa maendeleo ya Taifa. Amesema Serikali inaendelea kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 kwa kujenga uchumi imara, shindani na endelevu kwa kushirikisha rasilimali zote za kitaifa, ikiwemo rasilimali watu waliopo nje ya nchi.
Kwa mujibu wa waziri huyo, uhusiano kati ya Serikali na wanadiaspora umeimarika maradufu na umeanza kuzaa matunda katika nyanja za uwekezaji, uhamishaji wa ujuzi, ajira, utalii na maendeleo ya kijamii.
“Haya yote yanaonesha umuhimu wa ushiriki wa wanadiaspora katika kuharakisha maendeleo ya taifa letu, ndiyo maana Zanzibar inawaita wanadiaspora kuwekeza nyumbani,” amesema.
Akitaja takwimu, Dk Saada amesema zaidi ya Watanzania milioni mbili wanaishi nje ya nchi, kati yao, Wazanzibari wanakadiriwa kuwa kati ya 300,000 hadi 500,000.
Amesema mchango wao umeonekana moja kwa moja katika sekta za elimu, afya, biashara, makazi na utalii.
“Takwimu hizi zinaonesha uwezo mkubwa wa wanadiaspora kubadilisha uchumi wa taifa pale wanapoitikia wito wa kuwekeza nyumbani ipasavyo,” amebainisha.
Waziri huyo ametumia fursa hiyo kuwasihi wanadiaspora kujisajili kwa wingi ili Serikali iweze kuwatambua, kuwasikiliza, kuwashirikisha kitaalamu na kuwaunganisha na fursa mbalimbali za uwekezaji.
Aidha, amewahakikishia kwamba mfumo huo hauna dhamira ya kufuatilia maisha binafsi ya wanadiaspora, bali ni kwa ajili ya kuwatambua na kuwaunganisha na fursa zilizopo kwa maendeleo ya nchi.
Akitoa maelezo ya kiufundi kuhusu mfumo huo, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa na Uratibu wa Wazanzibari Wanaoishi Nje ya Nchi, Dk Haji Gora Haji amesema usajili wa wanadiaspora ulianza rasmi mwaka 2010 kwa kutumia mfumo wa makaratasi, hali iliyosababisha changamoto kubwa katika ukusanyaji na uhifadhi wa takwimu.
Amesema kutokana na changamoto hizo, serikali iliona umuhimu wa kuanzisha mfumo wa kidijitali wa ukusanyaji na uhifadhi wa taarifa za wanadiaspora katika kanzidata rasmi, hatua itakayoongeza ufanisi na kuondoa matumizi ya fomu za mkononi.
Dk Gora amesema mfumo huo umeanzishwa kwa ufadhili wa UNFPA kwa gharama ya Sh46 milioni.
Amesema mfumo huo umeundwa kwa kuzingatia urahisi wa matumizi, usalama wa taarifa na ufanisi.
Inaelezwa kuwa wanadiaspora wataweza kujisajili wakiwa popote duniani, huku taarifa zao zikitumika kwa madhumuni ya maendeleo ya Zanzibar kwa kuzingatia misingi ya faragha na usalama wa taarifa.
“Kupitia mfumo huu, Serikali itaweza kutambua maeneo wanayoishi wanadiaspora, taaluma na ujuzi walionao pamoja na maeneo wanayopenda kushiriki katika maendeleo ya Zanzibar,” amesema.
Hata hivyo, amesema mfumo huo tayari umeanza kufanya kazi rasmi na mwitikio ni mkubwa, ambapo hadi sasa wanadiaspora 1,312 wamekamilisha usajili wao.
Amewahimiza wengine kujisajili na kuwa mabalozi wa kuhamasisha wanadiaspora wa Zanzibar kujiunga na mfumo huo ili kupata taswira halisi ya rasilimali watu waliopo nje ya nchi.
Mwakilishi wa UNFPA, Ofisi ya Zanzibar, Ali Hamad amesema mfumo huo ni hatua ya kihistoria iliyoanza kujengwa tangu mwaka 2022, ikionesha dhamira ya Zanzibar ya kuunganika na watu wake walioko nje ya nchi. “Mfumo huu wa kuunganisha watu ni nguzo muhimu ya maendeleo endelevu,” amesema Hamad.
Akizungumza kwa niaba ya wanadiaspora, Suweid Yussuf Abdallah, mkazi wa Uingereza, amesema uzinduzi wa mfumo huo ulikuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu na sasa utekelezaji umeanza.
Ameipongeza serikali kwa kutambua na kuthamini mchango wa Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi kupitia sheria ya diaspora, akisema hatua hiyo inaonesha heshima na dhamira ya kweli ya kuwashirikisha katika maendeleo ya taifa lao.
Hata hivyo, Abdallah ametaja changamoto zinazohitaji kushughulikiwa haraka ili kuimarisha ushiriki wa wanadiaspora, ikiwemo suala la umiliki wa ardhi.
Amesema kwa sasa wanaruhusiwa kukodisha lakini si kumiliki moja kwa moja, hali inayokwamisha uwekezaji wa muda mrefu. Pia ametaja changamoto ya kukosa hadhi ya ukaaji wa kudumu au wa muda mrefu, jambo linalopunguza hamasa ya kuwekeza na kuwafanya wajisikie kama wageni.
Ameshauri Serikali kuendelea kufanya mikutano ya mara kwa mara na wanadiaspora ili kuboresha upatikanaji wa taarifa, kujenga imani na kuweka jukwaa rasmi la majadiliano kwa mujibu wa sheria ya diaspora.
Amesema hilo liende sambamba na kuhamasisha fursa za uwekezaji na mchango wa wanadiaspora katika maendeleo ya Zanzibar.