Mtoto wa Jenista Mhagama aibuka mshindi kura za maoni ubunge Peramiho 

Songea. Victor Mhagama, mtoto wa aliyekuwa Mbunge wa Peramiho, Mkoa wa Ruvuma, Jenista Mhagama ameibuka mshindi wa kura za maoni ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuwania ubunge wa jimbo hilo.

Mchakato wa uchaguzi  mdogo wa jimbo hilo, unafanyika kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Jenista aliyefariki dunia Desemba 11, 2025 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma baada ya kuugua maradhi ya moyo.

Victor anayetaka kuendeleza nyayo za mama yake ya kuwatumia wananchi wa Peramiho, ni miongoni mwa makada 27 walijitosa kuchukua fomu kuomba ridhaa ya CCM kupeperusha bendera katika uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika Februari 26, 2026.

Jana Jumatano, Januari 21, 2026, CCM Wilaya ya Songea Vijijini iliendesha kura za maoni kwenye kata 16 za jimbo hilo na Victor kuongoza.

Matokeo hayo yalitangazwa saa 5 usiku wa jana na
Mkurugenzi wa Uchaguzi  wa CCM, Wilaya ya Songea Vijijini, Juma Nambaila alimtangaza Victor kuwa mshindi kwa kupata kura 3,040 kati ya 8,577 zilizopigwa.


Amesema  kura zilizopigwa ni 9,167, kura zilizoharibika 590  na kura halali  ni 8,577.

Amewatangaza wengine na kura zao kwenye mabano ni Getrude Haule (2,913), Dk Joseph Mhagama (943), Frank Matola (215), Dk Lazaro Kiomba (213), Dk Damas Mapunda (200) na Isabellah Mwampamba(131).

Wengine ni Joseph Masikitiko (126), Erasmo Mwingira (124), Allen Mhagama (114), Schoral Ngonyani (84), Lazaro Ndenji(68), Davis Ngonyani(62), Thea Ntara (57), Emil Ngaponda (51), Serafina Mkuwa (48),Clemence Mwinuka (35), Emelian Mbawala (24), Benjamin Kamtawa(23), Prosper Luambano(22), Dominic Mahundi( 19),Fredrick Millinga (17),Sixmund Rungu (9),Rose Shawa (7),Rosemary Ngonyani(6),Enoc Moyo (6).


Amesema baada ya matokeo hayo vikao vya uamuzi ngazi ya wilaya,  mkoa na Taifa vitakaa na kuteua mwakilishi atakayewakilisha chama kwenye uchaguzi  huo mdogo.