KUNA fagio moja kubwa linaendelea Simba dirisha hili dogo la usajili hasa likihusu wachezaji wa kigeni huku timu hiyo ikishusha vifaa vipya.
Steven Mukwala, Jean Charles Ahoua, Moussa Camara, Chamou Karaboue na Joshua Mutale wote hawatokuwa na Simba katika miezi iliyobakia hadi msimu utakapomalizika.
Kipa Moussa Camara anawekwa nje ya orodha ya usajili hadi msimu utakapomalizika kwa vile bado hajapona majeraha na hajawa fiti kwa asilimia 100, Mukwala na Ahoua wameuzwa Kaskazini mwa Afrika huku ikisemekana Mutale na Chamou watatolewa kwa mkopo.
Kijiwe hakijashangaa Simba kuachana na Joshua Mutale na beki Chamou Karaboue na kwa mtazamo hao ni wachezaji ambao wamekuwa na bahati kubwa ndani ya Simba kwa kuweza kufika hadi katika dirisha hili dogo la usajili.
Kwa kile ambacho wamekifanya ndani ya timu hiyo tangu walipojiunga nayo, ilipaswa Simba iwe imeshawapa mkono wa kwaheri tangu katika dirisha kubwa la usajili mwaka jana kabla ya kuanza kwa msimu huu.
Tukianzia na Joshua Mutale, huyo ni kama bahati tu ilikuwa kwake hadi akasajiliwa na Simba kwa vile namba zake nchini Zambia hazikuwa za kuridhisha na alisajiliwa hapa nchini kwa vile aliisumbua tu Simba katika mechi mbili za mashindano ya klabu Afrika aliyokutana nayo wakati alipokuwa akiichezea Power Dynamos.
Simba aliendelea kutokuwa na mchango mkubwa kwani hakuwa mfungaji mzuri wala mtoaji pasi za mwisho zaidi alikuwa ni mchezaji msumbufu tu.
Chamou Karaboue naye alikuwa akifanya makosa mengi katika safu ya ulinzi ya Simba ambayo mara nyingine yaliigharimu timu.
Alicheza rafu ambazo hazikuwa na ulazima na kuna mechi alikuwa na bahati tu ya kutoonyeshwa kadi nyekundu au wapinzani kupata penalti.
Hatujui kama hao waliosajiliwa kuziba nafasi zao watafanya vizuri zaidi yao au la lakini kwa Mutale na Chamou kuachwa, Simba haijakosea chochote.