Mv New Mwanza kuzinduliwa kesho

Mwanza. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba anatarajiwa kuzindua safari za meli ya MV New Mwanza kesho Ijumaa, Januari 23, 2026, katika Bandari ya Mwanza Kusini, baada ya ujenzi wake kukamilika kwa gharama ya zaidi ya Sh120 bilioni.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi, Januari 22, 2026, jijini Mwanza, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema uzinduzi wa meli hiyo utaimarisha usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo katika Ziwa Victoria, sambamba na kuchochea shughuli za kiuchumi katika ukanda wa ziwa.

Profesa Mbarawa amesema kukamilika kwa ujenzi wa MV New Mwanza ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali pia ni kutimiza ndoto ya muda mrefu ya wananchi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa waliokuwa wakihitaji huduma ya uhakika na ya kisasa ya usafiri wa majini.

Amesema baada ya kukamilika kwa ujenzi, meli hiyo ilianza safari za majaribio Machi, 2025, zilizofanyika kwa awamu na vipindi tofauti, kwa lengo la kufanya tathmini ya kina ya utendaji wa mifumo mbalimbali ikiwemo injini, mifumo ya usalama na utendaji wa jumla kabla ya kuanza kutumika rasmi.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, baada ya kukamilika kwa majaribio yote muhimu, MV New Mwanza ilikaguliwa na Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac), ambalo liliiridhia na kutoa kibali cha kuanza safari za kibiashara.

“Hadi sasa MV New Mwanza imefanya jumla ya safari sita kati ya Mwanza na Bukoba kupitia Kemondo. Katika safari hizo, meli imebeba abiria 7,028 na kusafirisha mizigo yenye uzito wa tani 673.”

“Hatua hii imechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha usafiri na usafirishaji wa mizigo katika Ziwa Victoria,” amesema Profesa Mbarawa.

Ameongeza kuwa mafanikio ya safari hizo ni uthibitisho wa kukamilika kwa ujenzi wa meli hiyo kwa ubora uliosanifiwa na kuwa ni salama kwa utoaji wa huduma za usafiri wa abiria na mizigo majini, hivyo Serikali imeona ni wakati muafaka kufanya uzinduzi rasmi.

Meli ya Mv New Mwanza.



“Ninayo heshima kubwa kuwajulisha kuwa kesho, Januari 23, 2026, katika Bandari ya Mwanza Kusini, Waziri Mkuu atazindua rasmi kuanza kwa huduma za safari za meli hii. MV New Mwanza imeundwa kwa viwango vya kimataifa, ina urefu wa mita 92.6, karibu sawa na uwanja wa mpira wa miguu, upana wa mita 17 na kimo kinacholingana na jengo la ghorofa nne,” amesema Profesa Mbarawa.

Amefafanua kuwa wakati Serikali ya Awamu ya Sita inaingia madarakani, mradi huo ulikuwa umefikia asilimia 40 ya utekelezaji, huku mkandarasi akiwa amelipwa Sh40.644 bilioni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico), Eric Hamissi amesema matokeo ya safari za awali yanaonesha meli hiyo itajiendesha kwa kujitegemea na kuongeza mapato ya Serikali.

“Tumeona kupitia safari chache za majaribio kuwa meli hii ina uwezo wa kugharamia uendeshaji wake na kuleta tija kwa Serikali,” amesema Hamissi.

MV New Mwanza ina urefu wa mita 92.6, upana wa mita 17, uzito wa tani 3,500, ina ghorofa nne na uwezo wa kubeba abiria 1,200, mizigo yenye uzito wa tani 400 pamoja na magari 20, yakiwamo malori madogo na makubwa.

Meli hiyo inaendeshwa kwa kasi ya knoti 16, sawa na takribani kilomita 30 kwa saa, hali inayoiwezesha kufika Bukoba kwa muda wa saa sita hadi saba, ikilinganishwa na meli ya MV Victoria inayotumia takribani saa 10 kwa safari hiyo.

MV New Mwanza imegawanywa katika madaraja mbalimbali ya abiria kulingana na mahitaji na uwezo wao kiuchumi, yakiwamo daraja la hadhi ya juu (VVIP) lenye uwezo wa kuhudumia abiria wawili, daraja la watu mashuhuri (VIP) kwa abiria wanne, daraja la kwanza, daraja la biashara lenye uwezo wa abiria 100, daraja la pili kwa abiria 200 na daraja la uchumi linalobeba abiria 836.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema pamoja na uzinduzi wa MV New Mwanza, Waziri Mkuu pia atatembelea mradi wa ujenzi wa kituo cha kikanda cha uokozi na utoaji wa taarifa ndani ya Ziwa Victoria, pamoja na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa matenki ya maji mkoani humo.

Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo, sambamba na kusikiliza maelezo ya miradi mbalimbali itakayozinduliwa na kuwekwa jiwe la msingi na Waziri Mkuu.