Mvua yabomoa, kuezua nyumba tano Makambako

Njombe. Nyumba tano zilizopo mtaa wa Idofi, kata ya Mlowa, wilayani Makambako, Mkoa wa Njombe zimeezuliwa na ukuta kubomoka kutokana na mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali.

Kati ya nyumba hizo, mbili zimebomolewa jana Jumatano, Januari 21, 2026 ukuta na tatu zimeezuliwa paa na kusababisha wenye nyumba hizo kukosa makazi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Idofi, Cosmas Sambala amethibitisha kutokea kwa maafa hayo akisema wameweka utaratibu wa kuzisaidia kaya hizo kwa kila mwananchi kuchangia alichonacho.

“Baada ya mvua kunyesha hapo jana iliezua nyumba tatu na kubomoa nyumba mbili ina maana tano sasa wananchi waliponipigia simu nilifika eneo la tukio na kuona hiyo changamoto,” amesema Sambala.

Amesema baada ya kuona changamoto hiyo alimpigia simu diwani na kuweka mikakati ya kupiga ngoma ili wananchi wakusanyike kwenye eneo hilo na kuchangia walichonacho ili kupunguza adha iliyojitokeza.

Amewashukuru wananchi wa eneo hilo kwa kujitokeza na kuchangia ambapo mpaka sasa kwa kiasi kikubwa wameweza kupunguza changamoto iliyojitokeza isipokuwa nyumba moja ambayo tatizo lake ni kubwa.

Diwani wa Mlowa, Odilo Fute amesema kutokana na wananchi kuchangishana ili kuwasaidia waliokumbwa na changamoto ya nyumba zao kubomoka kutokana na mvua, zaidi ya Sh600,000 zilipatikana.

Amesema ametoa mifuko mitano kwa kaya mbili zilizokumbwa na changamoto ya nyumba zao kubomoka ukuta na bati 10 kila mmoja kwa waathirika wawili ambao nyumba zao zimeezuliwa.

“Tumembakiza mwananchi mmoja ambaye yeye ana changamoto kubwa zaidi tunaendelea kuomba wadau kumsaidia ili kumaliza changamoto iliyobaki kwani nyumba yake inahitaji zaidi ya bati 14,” amesema Fute.

Baadhi ya wananchi waliokutwa na maafa hayo akiwemo Mohamed Mduge ameomba kusaidiwa vifaa vya ujenzi hasa bati, misumari, mbao na matofali ili kujenga upya kuta ambazo zimebomoka na kuezeka nyumba zao.

“Changamoto tuliyokutana nayo ni kutokana na mvua za jana na upepo kwa hiyo zilinyesha sana na kuharibu miundombinu ya nyumba zetu ikiwemo kubomoka kuta na paa kuezuliwa,” amesema Mduge.

Naye Tusamehe Nyagawa ameomba mshikamano ulioonyeshwa na wananchi katika kuchangia pale inapotokea maafa kuendelea kusaidia pindi changamoto zinapotokea katika mtaa huo.