Mwenyekiti asimulia mtuhumiwa wa mauaji alivyomueleza tukio zima

Moshi. Tukio la mauaji ya kijana Mathias Teti (26), mkazi wa Kitongoji cha Kireiyo, Kata ya Uru Shimbwe, Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro, limewaacha wakazi wa eneo hilo na mshangao baada ya kudaiwa kuuawa kwa kukatwa na panga na baba yake mzazi, aliyetajwa kwa jina la Laurian Teti.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro iliyotolewa na Kamanda wa Polisi, Simon Maigwa, tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Januari 21, 2026, baada ya kuzuka kwa mvutano kati ya marehemu na baba yake kuhusu pombe ya posa ya dada yake ambaye aliolewa siku za hivi karibuni.

Inaelezwa kuwa marehemu alimdai baba yake pombe iliyokuwa imenunuliwa kwa ajili ya maandalizi ya kikao cha posa.

Kamanda Maigwa amesema baba wa marehemu anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuhusika na mauaji hayo na kwamba, upelelezi unaendelea, huku akibainisha kuwa mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya uchunguzi kukamilika.

Mwenyekiti wa Kitongoji asimulia tukio

Akizungumza na mwananchi leo Alhamisi Januari 22, 2026, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kireiyo, Emmanuel Kiwale amesema alipigiwa simu na mtuhumiwa usiku wa saa saba Januari 21, 2026, akimtaka afike nyumbani kwake akidai kuwa kulikuwa na tatizo kubwa.

“Aliniambia, ‘Mwenyekiti nakupa taarifa, hapa nyumbani kwangu kuna shida; nimemkata mtoto wangu mguu kwa panga.’ Nilipomuuliza kama amemkata sana, alisema amemkata vibaya kama mtu anavyokata mti,” amesimulia  Kiwale.

Amesema baada ya kupata taarifa hizo, alimpigia simu ndugu yake ambaye ni askari mgambo ili awahi eneo la tukio, huku akishindwa kupata usingizi kutokana na uzito wa taarifa alizozipokea.

Amesema baadaye alishindwa kumpata tena mtuhumiwa kwa simu, hadi alipopigiwa alfajiri na mtu mwingine akimjulisha kuwa kijana huyo hali yake ilikuwa mbaya na alikuwa amelazwa hospitalini.

Baadaye ilithibitika kuwa kijana huyo alifariki dunia kutokana na majeraha aliyoyapata.

Maldegunda Laurian, mama wa kijana anayedaiwa kuuawa na baba yake mzazi akizungumza na waandishi wa habari.



Baada ya kifo hicho, Mwenyekiti amesema waliamua kurudi nyumbani kwa marehemu kwa lengo la kuhakikisha mtuhumiwa asitoroke na  walifanikiwa kumkamata na kumfikisha Kituo cha Polisi Majengo.

Maelezo ya mtuhumiwa kwa mwenyekiti

Kiwale amesema walipofika nyumbani kwa marehemu walikuta damu nyingi zimetapakaa chini, ndipo alipomuuliza baba huyo kilichotokea.
“Aliniambia hapo ndipo alipomkatia panga na kwamba marehemu alikimbilia kwa mama yake akiwa amejeruhiwa,” amesema.

Kwa mujibu wa maelezo ya mtuhumiwa kwa Mwenyekiti, chanzo cha ugomvi kilihusisha madai ya marehemu kuwa pombe ya posa ya dada yake ikiletwa nyumbani hapo ataweka sumu ili waliokunywa wafe.

Mtuhumiwa alidai marehemu alianza kumtukana, kisha kumshambulia kwa jembe, hali iliyomfanya ahofie maisha yake ndipo alipochukua panga na kumkata mwanaye huyo mguuni mara mbili.

Aidha, mtuhumiwa alidai kuwa marehemu alikuwa akimtuhumu kwa kupokea posa za mara kwa mara kwa ajili ya dada yake.

Mama wa marehemu asimulia

Mama wa marehemu, Maldegunda Laurian amesema wakati wa tukio alikuwa amelala na alishtushwa na kelele za mwanaye aliyefika akiwa anatokwa na damu nyingi mguuni.

“Alikaa kwenye kochi, nilipotoka nje nikaona damu nyingi, nikapiga kelele kuomba msaada ndipo watu wakaja na kumpeleka hospitali,” amesema.

Akizungumzia madai ya pombe ya posa, mama huyo amesema hana taarifa zozote akieleza kuwa licha ya binti yao kuolewa, bado pombe ya mahari haijaletwa nyumbani.

Baba mdogo wa marehemu, Yusuph Teti amesema hakuwahi kupata taarifa za ugomvi wa marehemu na baba yake kuhusu suala la mahari, akieleza amesikia baada ya tukio kutokea.

Ameongeza kuwa, kwa mila na desturi, kaka hana haki ya kuhoji mahari ya dada yake kwa sababu  mamlaka hayo yapo kwa wazazi.

“Kaka hana haki ya kumuuliza baba yake kuhusu mahari ya dada yake. Alipaswa kusubiri kupewa taarifa na wazazi,” amesema.

Hata hivyo, familia imeeleza kuwa maandalizi ya mazishi yanaendelea na marehemu anatarajiwa kuzikwa Jumamosi nyumbani kwao Uru Shimbwe, Wilaya ya Moshi.